Friday, January 30, 2009

MAWAZO THABITI YENYE MSIMAMO THABITI.

MWANACHAMA.

Wiki hii nimejiunga na Chama cha kisiasa, nimepata kadi yangu ya uanachama wa CCM. Hatua hii haikuwa ndogo maana nina rafiki yangu ambaye alinilaumu na kunitukana ati kwa nini najiunga na CCM wakati ni chama kibovu kwa mtazamo wake. Nikamwambia mie mtu mzima na nina maamuzi yangu. Alinicheka tu na kuniita “mtu mzima ovyo”.
Lakini swali alilouliza rafiki yangu Ngoge wakati tupo kwenye mkutano wa kukabidhiwa kadi zetu ni kwamba sisi sote tuliopo nje ya Tanzania baada ya kujiunga na CCM, tuna nia gani za kujiunga na kama zipo tutatimiza vipi nia hizo. Swali hili kwa kweli lilileta mtafaruku maana kila mtu aliongea lake na ubishi ulikuwa juu!
Nia za kujiunga zilizotamkwa na watu zilikuwa nyingi. Zao mzee wa kinywaji alisema yeye kajiunga ili awe salama, “haujui huko mbele itakuwaje, lazima ujikinge na kikadi” ndivyo alivyosema Zao. Manembo yeye alisema kajiunga kwa kuwa hakuna chama kingine cha siasa chenye uongozi walau madhubuti, nchi nae yeye anapenda sana kushiriki kisiasa na ana mchango mkubwa sana kwa Tanzania na sista duu Katrina yeye hakuwa na aibu alisema waziwazi kuwa yeye kafuata mkumbo, “shoga yangu kajiunga na mimi nimejiunga, kuna ubaya?” alisema na kuuliza Katrina. Kwa kweli nia zote ni nzuri, na mimi siwezi kumuhukumu mtu yeyote kuhusu nia yake ya kujiunga ili mradi nia haisababishi matatizo kwa mwingine, kama wanavyosema waswahili “nia ni nia tu”
Lakini nia aliyoisema Majuto ilinivutia kidogo. Yeye alisema anataka kuiendeleza nchi yetu Tanzania na kwa mtazamo wake alisema itakuwa rahisi sana kufanya mabadiliko nchini kupitia CCM maana ni chama chenye maadili na mapenzi mema kwa wananchi ambayo viongozi wake wote wakiyafuata nchi ya Tanzania itaendelea na kubadilika sana. Alisema nia yake ni kuendeleza umoja na mshikamano na kuleta maendeleo kwa yeyote ambaye ataweza kumgusa, aliongea mengi sana mazuru na kila mtu alivutiwa sana na alichosema.
Mgema ambaye alikuwa kimya kwa muda kidogo alifumbua kinywa na kuja na hoja iliyochangamsha wote waliopo. Yeye alisema nia zote tulizonazo sisi tuliojiunga na CCM nje ya nchi ni nzuri lakini kama hatuna mikakati ya kuzitimiza, nia zote ni bure. Alisema lazima tuwe na mikakati ya kuzitimiza ili nia zisiwe ndoto tu bali ziwe ndoto zilizogeuka kuwa kweli.
Sasa hapa ndio shida inapokuja, maana moja ya matatizo ni kwamba tupo mbali na nje ya Tanzania, na wahenga wanasema fimbo ya mbali haiui nyoka. Lakini Katrina hakukubaliana na huu msemo na akaja na agenda kwamba mtu mwenye shabaha anaweza kuirusha hiyo fimbo na ikatua katikati ya kichwa cha nyoka na kumuua, kila mtu alicheka. Swali likawa je ni mikakati gani waliyonayo waliopo nje ya Tanzania, wenye kadi za CCM na wanataka kuendeleza Tanzania katika njia moja au nyingine, wanaweza kuitumia ili kuleta maendeleo?
Kimoja alichosema Majuto ni kuwekeza Tanzania. Alisema tutaisaidia sana Tanzania kama tutapeleka fedha za kigeni na kuwekeza Tanzania aidha kwa kumsomesha ndugu, jamaa na marafiki, kwa kununua hisa au kuanzisha biashara. Ila alionya kuwa hili si swala dogo na pia linahitaji uchunguzi, uaminifu na utumiaji wa akili na hekima, ila linawezekana. Mgema yeye alisema sisi wa nje tunaweza kuwaelimisha na kupata elimu kutoka kwa wenzetu wa nyumbani kwa kutumia teknolojia mbalimbali. Alisema kwa kutumia teknolojia tunaweza pia kuitangaza nchi yetu ili watalii wakaenda kuitembelea na watu wanaoweza kuwekeza wakaenda kuwekeza.
Jambo kubwa ambalo lilizua mzozo alilizungumza Ngendewa. Yeye alisema nia yake ya kujiunga na CCM ni kurudi nyumbani na kusaidia iwezekanavyo. Magambo alimrushia kijembe kuwa asitegemee eti kwa kuwa yeye yupo nje basi akirudi Tanzania atapata ubunge. Hata hivyo Ngendewa alisema kama yeye anataka kwenda nyumbani akawe mbunge atakuwa chizi maana kwanza amekaa nje muda mrefu na hajua kwa undani matatizo na matakwa na mengi tu ya watu, hivyo akiwa mbunge hatakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuongoza. Alisema yeye anakwenda ili ajiweke karibu na wananchi, awasaidie na wamsaidie kwa namna moja au nyeingine, anajiweka karibu na matatizo wanayoyakabili Watanzania na karibu na kuyatatua, anajiweka karibu na watu watakaoweza kunufaika na elimu yake ya nje nay eye kunufaika na elimu ya Watanzania, anajiweka karibu na hali nzuri ya kuchunguza na kufahamu vitega uchumi nyenye faida ili kuwekeza, na anajiweka karibu na kuleta maendeleo na kukemea maovu.
Kila mtu aliona Ngendewa ameongea la maana, lakini Ngendewa aliuliza je kuna mtu yeyote atakuwa tayari kuungana naye kurudi nyumbani, wote tukawa kimya. Oh! mimi naitwa Mwisomba.


Freddie Mwisomba.
United state of america.

3 comments:

Anonymous said...

Ndugu mwanachama ujumbe wako tumeupata, pia tunakuomba uwe mwanachama mzuri mwenye mtizamo wa kusaidia nchi yako.

Anonymous said...

Ndugu tunajua unataka ubunge. Njoo upambane na kutueleza mikakati uliyo nayo

Anonymous said...

wewe umeishapewa rushwa na hao viongozi wa ccm marekani hili usema wanachotaka kukisikia. Ukija bongo tunakutoa mbio.