Thursday, March 15, 2012

MKUTANO WA KAMPENI ZA CCM ARUMERU LEO MACHI 14


Meneja kampeni za CCM,uchaguzi mdogo Arumeru Mashariki, Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha CCM, Mwigulu Nchemba (kulia) akimnadi mgombea wa CCM jimbo hilo, Sioi Sumari katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo, 14/3/12 katika kijiji cha Shambarai, Kata ya Mbuguni.(Picha zote na Bashir Nkoromo).
Wananchi wa kijiji cha Shambarai, Kata ya Mbuguni, wakishangilia wakati wa mkutano wa kampeni za CCM za uchaguzi mdogo jimboni humo leo.
Mgombea ubunbge wa CCM jimbo la Arumeru Mashariki, Sioi Sumari akiwaalimia wakati wa kijiji cha Shambarai Kata
ya Mbuguni kabla ya mkutano wa kampeni za CCM leo.
Pamela Sioi akimuombea kura mumewe, mgombea ubunge wa CCM, jimbo la Arumeru Mashariki, Sioi Sumari kwenye kampeni zilizofanyika kijiji cha Shambarai kata ya Mbuguni jimboni humo leo.
.Mama Sioi(wapili kulia) akishiriki kuselebuka muziki wa hamasa za Chama, uliporomoshwa katika kijiji cha Msitu wa Mbogo kata ya Mbuguni kabla ya kuanza kampeni za CCM za uchaguzi mdogo jimboni humo leo.
Sioi Sumari akiwaaga wapigakura wake baada ya kumaliza mkutano katika kijiji cha Msitu wa Mbogo, leo.

Tuesday, March 13, 2012

Kishindo kampeni CCM, Mkapa Kivutio

Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Benjamin Mkapa akimnadi Mgombea wa Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya chama hicho, Sioi Sumari (kushoto) kwa wananchi wa Usa River kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho zilizofanyika kwenye Uwanja wa Ngaresero, jijini Arusha.


Mji wa Usa River katika Wilaya ya Meru jana ulitikiswa na kishindo cha uzinduzi wa kampeni za CCM, ulioongozwa na Mwenyekiti wake Mstaafu, Benjamin Mkapa.Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Ngaresero, Mkapa alikanusha kuwa na ubia na kampuni ambazo zimewekeza katika maeneo makubwa ya ardhi ya Meru.Suala la migogoro ya ardhi ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayowakabili wananchi wa wilaya hii na jana Mkapa alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kukanusha kwamba ana ubia na wale aliowaita kuwa ni walowezi katika wilaya hiyo.

“Kwanza kabisa nataka niweke mambo sawa, nimesikia kwamba ninahusishwa na hawa wamiliki wa ardhi, eti kina nani hawa… ndiyo Jerome sijui Jerome, huu ni uzushi na hauna ukweli wowote,” alisema Mkapa alipokuwa akimnadi mgombea wa CCM, Sioi Sumari na kuongeza:

“Mimi katika nchi hii sijawahi kumpokonya mwananchi yeyote shamba, wala kumnyanyasa Mtanzania yeyote kwa kumpokonya ardhi, nimekuwa mtetezi wa kuhakikisha kila watu wanapata haki ya matumizi yao ya ardhi, haya maneno mengine ni uzushi na upuuzi wa hali ya juu.”

Alisema amepokea taarifa za kuwapo kwa migogoro mikubwa ya ardhi inayosababishwa na baadhi ya wawekezaji kuhodhi maeneo makubwa na kusema atalifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na kumshauri achukue hatua kwa kuwawajibisha watendaji wa Serikali ambao wameshindwa kuwajibika na kuchukua hatua kwa wawekezaji waliokiuka masharti.

“Yapo matatizo kadha wa kadha, wapo wawekezaji ambao wamehodhi maeneo makubwa wakati hawayatumii, wapo ambao wamechukua maeneo na kubadilisha matumizi yake na wapo ambao wamekiuka sheria za uendeshaji wa maeneo waliyopewa,” alisema Mkapa na kuongeza:

“Yote haya nimeyapokea na nitayafikisha kwa Mwenyekiti wangu wa CCM ambaye pia ni Rais wangu ili ayashughulikie baada ya uchaguzi maana tukifanya sasa, hawa wenzetu (wapinzani) watasema tumewahonga wananchi.”

Aidha, Mkapa alikanusha taarifa kwamba alitoa masharti baada ya kuombwa kuongoza uzinduzi wa kampeni hizo za CCM: “Mimi ninamheshimu sana Mwenyekiti wangu wa CCM na uamuzi wa Kamati Kuu ya chama maana nimezaliwa CCM na kukulia ndani ya CCM. Kwa maana hiyo siwezi hata siku moja kuhoji au kutoa masharti pale ninapoombwa na chama kutekeleza jukumu lolote.”
Shamrashamra
Shamrashamra za CCM zilianza asubuhi kwa magari na pikipiki zilizopambwa kwa bendera za kijani na njano kupita katika mitaa mbalimbali ya Usa River, zikiwahamasisha wakazi wa mji huo kuhudhuria uzinduzi huo.
Mapema viongozi kadhaa wa chama hicho walitawanyika katika kata zote 17 za Arumeru Mashariki kulifanya mikutano ya ndani kwa lengo la kuwaweka sawa makada wao ambao wanadaiwa kuchanganywa na taarifa kwamba chama hicho kimegawanyika kuhusu mgombea wao, Sioi Sumari.

Baadaye mchana, msafara wa mgombea huyo wa CCM ulianza kuelekea katika eneo la mkutano ukitokea katika Hoteli ya Gateway ukisindikizwa kwa magari na pikipiki.

Kabla ya msafara huo kuondoka, kulikuwa na kikao cha ndani kilichofanyika hotelini hapo kikiwahusisha viongozi wa chama hicho na taarifa za ndani zinadai kwamba kilikuwa kikipanga mikakati ya mkutano huo wa uzinduzi.

Msafara huo ulitoka hotelini hapo saa 9.15 alasiri na kuingia Barabara Kuu ya Arusha-Moshi, njia ya Leganga na kuelekea moja kwa moja katika Ngarasero.
Wakati msafara huo ukiwa Barabara ya Leganga ukielekea uwanjani, ulipita karibu na kambi waliyofikia viongozi mbalimbali wa Chadema na baadhi ya makada wa chama hicho walijitokeza na kuzomea msafara huo.

Msafara huo uliwasili uwanjani hapo robo saa baadaye na viongozi wake waliungana na wanachama wao waliokuwa uwanjani hapo tayari kwa uzinduzi.

Wapinzani wa Sioi
Katika uzinduzi huo, CCM kiliwapandisha jukwaani baadhi ya wanachama wake waliokuwa wapinzani wa Sioi kwenye kura za maoni. Makada hao ni Elishilia Kaaya, Elirehema Kaaya na William Sarakikya na wote waliuthibitishia umma kumuunga mkono mgombea huyo wa CCM.

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa aliwaomba wana Arumeru Mashariki kulinda mila na desturi iliyojengeka ndani ya taifa kuwa inapotokea kiti cha uongozi kama ubunge kinachomilikiwa na CCM inabaki wazi, mrithi atoke ndani ya chama hicho.

“Mila na desturi zinataka mrithi wa kiti kinachomilikiwa na CCM kirithiwe na mrithi kutoka CCM. Mchagueni Sioi kutekeleza hilo ili ashirikiane na wenzake bungeni kutatua matatizo yenu,” alisema.

Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama alisema tayari chama hicho kimetekeleza ahadi na deni kililokuwa nalo kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Jeremia Sumari ambaye ni baba mzazi wa Sioi kwa kulipa Jimbo la Arumeru Mashariki hadhi ya kuwa wilaya kamili kichama.

Vijembe kwa Chadema
Meneja wa kampeni za CCM Arumeru Mashariki, Mwigulu Nchemba aliwapiga vijembe viongozi wa Chadema akimwomba Mkapa kumsihi Rais Kikwete awateue Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi ili wasije kulalamika pale mgombea wao atakaposhindwa.

Mwigulu alitumia maneno mengi ya kejeli kwa Chadema na mgombea wake, Joshua Nassari kwa kumfananisha na vitu kama shetani, gunzi na vinyamkera huku akiwasihi wapiga kura kutomchagua mgombea huyo.

Nchemba ambaye pia ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM, alisema CCM kina uhakika wa ushindi katika jimbo hilo kwani mgombea wake, anakubalika.

Alisema licha ya kuwepo matatizo kadhaa Arumeru, hoja si kusema kwa ukali, bali ni kuwa na mipango ya kukabiliana na matatizo hayo... “Chagueni mtu ambaye atasikilizwa na Serikali na mtakayeshirikiana naye kutatua matatizo na sio mtu ambaye anasema kwa ukali ambaye anapotosha jamii.”

Kuhusu uchangishaji wa fedha uliofanywa na Chadema wakati wa uzinduzi wa kampeni, alisema ni kejeli kwa wananchi kuwachangisha Sh50 wakati wanatumia helikopta ambayo kwa saa moja angani gharama zake ni Sh2.5 milioni na Sh15 milioni kwa siku.

Ahadi za baba
Mgombea huyo wa CCM, alisema kipaumbele cha kwanza akichaguliwa ni kutekeleza ahadi zote alizoacha baba yake... “Najua nina deni kwenu, mkinichagua nitahakikisha ninakamilisha ahadi zote za baba kama kukamilisha Barabara ya Ngabobo, ujenzi wa nyumba ya wazee wa mila, kukamilisha ujenzi wa vyoo katika shule na kukamilisha ujenzi wa Shule ya Wasichana ya Songoto.”

Mgombea huyo pia alisema ajenda kubwa ambayo atatekeleza baada ya kuchaguliwa itakuwa ni kushughulikia matatizo ya maji na ajira kwa vijana katika jimbo hilo.

Monday, March 12, 2012

MKAPA KUONGOZA UZINDUZI WA KAMPENI ARUMERU





Wajumbe wa kamati kuu CCM wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa kupitisha jina la Sioi Sumari kugombea jimbo la Arumeru
























RAIS Mstaafu, Benjamin Mkapa leo anatarajiwa kuongoza uzinduzi wa kampeni za CCM za uchaguzi mdogo wa ubunge Arumeru Mashariki zitakazofanyika katika Kata ya Usa River, wilayani Meru, Arusha.

Uzinduzi wa kampeni za CCM unakuja siku moja tangu wapinzani wao wakuu, Chadema wazindue kampeni katika Uwanja wa Leganga, Usa River wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Vyama hivyo viwili vyenye upinzani mkubwa nchini, vinatarajiwa kubeba ajenda mbili kuu; migogoro ya ardhi na uhaba wa upatikanaji maji kwa matumizi ya nyumbani na kilimo.

Baadhi ya wakazi wa Arumeru wanasema mbunge wanayemtaka ni yule atakayeweza kuwaondoa katika migogoro ya ardhi ambayo inachochewa na maeneo makubwa kuchukuliwa na wawekezaji.

Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba viongozi mbalimbali wa kitaifa watakuwa na vikao vya ndani katika kata zote 17 za jimbo hilo.

“Tayari tumekutana na makundi yote na sasa hali ni shwari. Makundi yote yameungana kumuunga mkono mgombea wetu Siyoi Sumari ambaye tuna uhakika atashinda,” alisema Chatanda.

Awali, kulikuwa na utata kama Rais mstaafu huyo, atafika kuzindua kampeni hasa kutokana na mpasuko mkubwa wa viongozi uliotokana na kura za maoni na makundi ya wanaojipanga kuwania urais mwaka 2015.

Alisema uzinduzi huo utahudhuriwa na viongozi kadhaa, akiwemo Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama na Mlezi wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Stephen Wassira... “Kabla ya uzinduzi ambao utaanza majira ya saa 9:00 alasiri, kutakuwa na maandamano ya wafuasi wa CCM kutoka nyumbani kwa mgombea wetu eneo la Akheri hadi Usa River. Hatutaraji kuleta watu kutoka Arusha au Hai kama wenzetu (Chadema), sisi tutakuwa na watu wa Arumeru na watajaa uwanjani.”


Monday, March 5, 2012

CCM, Chadema sasa vita rasmi

Rais wa awamu tatu, Benjamin Mkapa


VYAMA vya CCM na Chadema vimetangaza rasmi vita ya kuwania Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha huku vikianika majina ya makada watakaoongoza mapambano kwa ajili ya kujihakikishia ushindi.CCM ambayo imempitisha Siyoi Sumari kuwania nafasi hiyo, imesema kampeni zake zitazinduliwa na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho ambaye pia alikuwa Rais wa awamu tatu, Benjamin Mkapa na Chadema itawatumia viongozi wake wa kitaifa, wakiongozwa na Mwenyekiti wake Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa.

Wakati huohuo, Kamati Kuu (CC) ya Chadema jana ilimpitisha, Joshua Nasari kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo. Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Mbowe aliwaeleza viongozi wakuu wa chama hicho, wapenzi na wafuasi wa Chadema waliojazana eneo la Hoteli The Ice Age Usa-River, wilayani Arumeru jana kuwa wamejiandaa kikamilifu kunyakua jimbo hilo na kamwe hawatakubali hujuma zozote kutoka kwa mtu au chama chochote. Mbowe aliyezungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wake, Dk Slaa kumtanga rasmi Nasari, alitamba kuwa mchakato wa kumtafuta mgombea kupitia chama hicho haujaacha nyufa wala mifarakano miongoni mwa wagombea na wafuasi wao kama ilivyotokea kwa vyama vingine vya siasa ambavyo hakuvitaja. Alisema mara nyingi mipasuko ndani ya vyama vya siasa hutokana na mchakato wa kupata wagombea kutokana na hila za baadhi ya viongozi, wanachama au wapambe wa wagombea, hali aliyosema haijajitokeza ndani ya Chadema kutokana na mfumo mzuri unaozingatia demokrasia kwa wote bila kujali umaarufu au ukwasi wa mtu.“Wagombea wote waliojitokeza kuchukua fomu kuomba uteuzi tumewaalika katika Kamati Kuu na wote wameridhika na ushindi na uteuzi wa mgombea mwenzao na wote watashiriki kikamilifu kwenye kampeni kuhakikisha ushindi wa chama unapatikana,” alisema Mbowe.

Akitangaza uamuzi wa Kamati Kuu, Dk Slaa, alisema kikao hicho kilichoshirikisha wabunge, mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya zinazoongozwa na Chadema, kwa kauli moja kilipitisha jina la Nasari kuitikia sauti ya wananchi na wakazi wa Arumeru waliomchagua kwa kura 805 kati ya 888 zilizopigwa kwenye kura za maoni. “Wananchi Arumeru tumesikia kauli yenu kupitia kura zenu za maoni, Nasari ni kijana wenu siyo wa Dk Slaa, Mbowe wala Chadema. Katika kura za maoni, Nasari alimwacha mbali mgombea wenzake Anna Mghiwa aliyemfuatia kwa kupata kura 23 huku wagombea wengine wanne, wakipata kura chini ya 20. Chama hicho pia kinaendelea kufanya tathimini ya kutumia helikopta katika kampeni zake katika jimbo hilo.Nasari ashukuruAkitoa shukrani mbele ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama chake, Nasari aliwaomba wafuasi, wapenzi na wanachama wote wa Chadema kushikamana na kuwa tayari kwa mapambano ya haki, kuhakikisha wanaibuka na ushindi mnono kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa."Wao (CCM), najua watatumia dola na fedha, lakini sisi tusihofu kwani tuna Mungu anayetupigania kwa sababu mapambano yetu ni kudai haki dhidi ya uovu. Kwa pamoja tukishirikiana kuondoa hofu kwani tutashinda," alisema Nasari.

Kwa upande CCM Kamati Kuu (CC) ya chama hicho jana ilimteua Mwenyekiti mstaafu ambaye pia ni Rais mstaafu wa awamu ya Tatu , Mkapa, kuongoza kampeni za kumnadi Mgombea Ubunge wa chama hicho, Siyoi Sumari katika jimbo la Arumeru Mashariki.Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye, alisema kikao cha kamati hiyo kilichoketi jana, kilipitisha jina la Siyoi kuwania nafasi hiyo iliyoachwa na baba yake, Jeremia Sumari aliyefariki usiku wa Januari 18 mwaka huu.Nape alieleza kwamba, kamati hiyo pia imemteua Katibu wa Idara ya Uchumi na Fedha ya chama hicho, Mwingilu Nchemba kuratibu kampeni hizo.Katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga ambao CCM ilishinda, Mkapa ndiye aliyefungua kampeni hizo huku, Nchemba akiratibu kuanzia mwanzo hadi mwisho.Akizungumzia tuhuma za rushwa ambazo zimekuwa zikiripotiwa katika mchakato wa uteuzi, aliitaka Takukuru kuhakikisha wanakamata mtandao mzima uliohusika na utoaji rushwa.Kauli ya Siyoi Sumari, aliambia Mwananchi Jumapili kuwa kwamba pamoja na kufurahishwa na uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kupitisha jina lake kupeperusha bendera ya CCM wilayani Arumeru Mashariki, chama hicho kinapaswa kutoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha kinatetea jimbo hilo. Hata hivyo, alisisitiza kwamba changamoto zote alizozipitia katika mchakato wa uteuzi , zikiwemo tuhuma mbalimbali za rushwa ni misukosuko ya kisiasa ambayo haiwezi kuepukwa zaidi ya kukabiliana nayo. “Nashukuru chama kwa kupitisha jina langu, lakini changaomoto zote nilizokuwa nikipitia naamini ni misukosuko tu ya kisiasa, lakini tusahau yaliyopita sasa tusonge mbele kunyakua ushindi,” alisema Sumari

UVCCM
Katika hatua nyingine Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM ) wilayani Arumeru, imefurahishwa na uamuzi uliofanywa na CC ya CCM kumpitisha Siyoi kupeperusha bendera ya chama hicho na kueleza kwamba kilio cha wanachama wa CCM wilayani humo, sasa kimesikilizwa. Hata hivyo, wakati jumuiya hiyo ikiupokea ushindi huo kwa furaha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) imeendelea na kamata kamata yake ambapo safari hii ilimshikilia na kumhoji kwa muda Katibu Hamasa wa umoja huo wilayani Arumeru Mashariki, John Nyiti kisha kumwachia huru. Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Esther Maleko alisema mbali na kilio cha wakazi wa jimbo hilo kusikika juu ya mgombea wao, umoja wao umejipanga kikamilifu kuingia ulingoni kuhakikisha ushindi unapatikana. Hekaheka za uchaguzi wa jimbo hilo wakati zikiendelea baadhi ya makada wa CCM na UVCCM wilayani humo wameendelea kukumbwa na misukosuko baada ya viongozi wake akiwemo Nyiti kushikiliwa na Takukuru kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa wilayani humo. Nyiti alipoulizwa juu ya taarifa hizo kwa njia ya simu alikiri kukamatwa na maofisa wa Taasisi hiyo. Kamanda wa Takukuru mkoani Arusha, Mbengwa Kasumambuto alipoulizwa na gazeti hili juu ya taarifa hizo hakuweza kukiri wala kukataa juu ya kuhojiwa kwa kada huyo na kudai kwamba wanaohojiwa na Taasisi hiyo wako wengi na wengine wanahojiwa kama mashahidi, hivyo alidai si vyema kuwataja majina kwa kuwa bado wanakamilisha uchunguzi wao.

Hali ilivyo ndani ya vyama
Makundi ya vigogo wa CCCM ambao wanajipanga kugombea Urais mwaka 2015, yametajwa kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama hicho katika uteuzi wa mgombea wa Ubunge Arumeru Mashariki.Mpasuko wa makundi hayo, inaelezwa unaweza kuchangia chama hicho kupoteza jimbo hilo.Sumari amekuwa akiungwa mkono na kundi la Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa huku wagombea wengine, walikuwa wakiungwa mkono na kundi la na vigogo wa chama hicho wanaojipambanua kuwa ni wapiganaji dhidi ya ufisadi.Wakizungumza na Mwananchi Jumapili jana katika mahojiano maalumu baadhi ya viongozi wa CCM na makada wa Chama hicho, wameeleza mpasuko huo ni mkubwa tofauti na wengi wanavyofikiri.Asantaeli Erio alifafanua kuwa, kwa sasa baada ya Sumari kupitishwa, kundi la vigogo wa CCM na Serikali huenda wakasusa kumpigia kampeni hasa kutokana na kubainika wazi kutomuunga mkono na siri za hoja zao kuvuja. Wafuasi wa Sarakikya Kundi la wafuasi wa aliyekuwa mgombea wa ubunge wa CCM, William Sarakikya na Elishilia Kaaya jana, walieleza kutokubaliana na maamuzi ya Kamati Kuu kupitisha jina la Sumari kuwania jimbo hilo.Mmoja wa wafuasi hao, Emanuel Kanangira alisema wanapinga uteuzi wa Sumari na leo wanatarajia kurejesha kadi za CCM.

Upande wa Chadema
Ingawa Joshua Nasari ndiye amepitishwa kuwania nafasi hiyo ya ubunge, huenda ushindi wa Chadema katika jimbo hilo, ukawa mgumu kutokana na viongozi wa koo za kabila la Kimeru maarufu kama 'Washili' ambapo wengi wanatoka familia ya Sumari kutangaza mgogoro na chama hicho.Viongozi hao kupitia Mwenyekiti wao,Chief Sumari kutangaza kumzuia Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini, Godbless Lema ambaye alitarajiwa kuwa meneja kampeni wa Chadema katika jimbo hilo, kutua Arumeru wakimtuhumu amewakashifu.Hata hivyo, mmoja wa wazee wa kabila hilo, Yohane Kimuto alitangaza juzi kupinga kauli hiyo na kusisitiza Lema atafika Arumeru na kufanya kampeni.

Sunday, March 4, 2012

Kikao cha Kamati Kuu ya CCM

Mwenyekiti wa CCM, Rais Dr.Jakaya Mrisho Kikwete,Makamu wa Rais Dr.Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa pili wa SMZ Balozi Seif Iddi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakijadili jambo muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati kuu ya Halmashauri kuu ya CCM ilichofanyika ikulu jijini Dar es Salaam

Saturday, March 3, 2012

MGOMBEA WA UBUNGE-ARUMERU MASHARIKI KWA TIKETI YA CCM


Sioi Sumari
Mgombea Rasmi wa CCM- Arumeru Mashariki