Thursday, April 2, 2009

MTAMBO WA SONGAS KUANZA UZALISHAJI NDANI YA MAJUMA MAWILI

Waziri ngeleja akiongea na wana habari katika moja ya mikutano yake.
Serikali imesema kuwa ndani ya wiki moja kuanzia tarehe 28/03/2009 mtambo wa kuzalisha umeme wa Kampuni ya Songas ulioharibika utakuwa tayari na kuanza kufanya kazi kama kawaida.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja alipofanya ziara ya kutembelea mitambo hiyo iliyopo Ubungo jijini Dar es Salaam ili kuona maendeleo ya matengenezo ya mitambo miwili iliyosababisha upungufu wa megawati 50 za umeme katika gridi ya Taifa.

“Kwa taratibu za kawaida matengenezo ya mtambo huu yangechukua miezi mitatu hadi minne ila mafundi wanafanya kazi ya matengenezo kwa bidii na hatua waliyofikia watachukua muda mfupi kumaliza kazi hii”, alisema waziri Ngelleja.

Aliendelea kusema kuwa mgao unaoendelea ni kutokana na ajali ya kuharibika kwa mtambo mmoja kwani mtambo mwingine uko katika matengenezo ya kawaida ila baada ya kuharibika kwa mtambo huo ndiyo tatizo limeongezeka zaidi.

Ngelleja alisema kuwa, “Serikali haina mpango wa kuwafanya wananchi waishi gizani zipo hatua nyingi ambazo wanazichukua na watazitolea ufafanuzi kadri siku zinavyokwenda”.

Mtambo wa pili wenye uwezo wa kuzalisha megawati 35 ambao uko katika matengenezo ya kawaida unatarajia kuanza kazi baada ya wiki mbili tangu kuanza kwa matengenezo hayo.

Hivi sasa mtambo ulioharibika umefumuliwa na kuanza kutengenezwa upya na una uwezo wa kuzalisha megawati 20 za umeme kama utaanza kazi utakuwa umepunguza makali ya mgao wa umeme kwa kiasi fulani.

Kuanzia Alhamisi wiki hii jijini Dar es Salaam kumeanza mgao wa umeme ambao unaleta usumbufu kwa wananchi hii ni kutokana na kuharibika kwa mitambo hiyo .

Msomaji
Dar es salaam

No comments: