Tuesday, July 28, 2009

Idadi ya watalii wanaoingia nchini Tanzania yazidi kuongezeka

Dk Ladislaus Komba
Pamoja na mtikisiko wa uchumi unaoendelea duniani, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Ladislaus Komba amesema tathmini ya awali ya biashara ya utalii nchini inaonyesha kuwa idadi ya watalii inaongezeka hapa nchini kama ilivyopangwa.
Dk Komba alisema hali hiyo inaweza kuendelea kuwa nzuri ikiwa huduma na miundombinu katika maeneo ya utalii itaboreshwa na kutoa unafuu kwa watalii. Alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alisema tathmini inaonyesha kuwa idadi ya watalii inazidi kuongezeka na kwamba kinachotakiwa kufanywa na serikali kwa sasa, ni kuondoa baadhi ya kasoro za huduma kwenye sekta hiyo. "Watalii wengi wanaokuja Tanzania kwa sasa ni kwa ajili ya mapumziko na wengi wanatoka Marekani, Uingereza, Ujerumani na Italia", alisema.
`Watalii wameongezeka kwa asilimia 11.6 katika (kipindi cha mwaka 2007/2008) na pato linalotokana na matumizi ya kitalii nalo limeongezeka kwa asilimia 26, ukilinganisha na mwaka 2006,`` alisema Dk Komba wakati akiwa anahudhuria mkutano wa wadau wa sekta ya utalii katika kujadili tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu serikalini.
Maelezo ya Dk Komba yamekuja wakati ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga akisema serikali inatathmini mfumo wa utalii kwa ujumla ili kuangalia kama kuna uwezekano wa kupunguza gharama za kitalii au la.
Hii ilitokana na shinikizo kutoka kwa baadhi ya wadau wa sekta binafsi wa utalii kuitaka serikali kupunguza gharama hizo kama ilivyofanya
Kenya hivi karibuni ili kuwavutia watalii wanaoshindwa kuja kutokana na kuathirika kifedha baada mtikisiko wa kiuchumi duniani. Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Tafiti, Mafunzo na
Takwimu wa wizara hiyo, Ibrahim Mussa alisema maboresho mengine yanayopaswa kufanywa ni kuweka mashine za kutoa fedha kwa njia ya viza, kwenye vituo vya utalii.
''Unajua mara nyingi watalii hawapendi kutembea na fedha taslimu, wanataka hata wakifika kwenye mahoteli baada ya kutumia wakae na fedha zo kwenye kadi zao,`` alisema Mussa.
Msomaji
Dar es salaam

1 comment:

Anonymous said...

Sasa kama idadi ya watalii wanaoingia nchini inaongezeka mbona mabadiliko yake hayaonekani kwa walengwa?