Monday, July 27, 2009

WAGONJWA TARAFA YA KATERERO MKOANI KAGERA WALALA NA MAITI WODINI

Katoro Wagonjwa wa kijiji cha Katoro kata ya Katoro Tarafa ya Katerero wilaya ya Bukoba vijijini wanaolazwa katika kituo cha afya Katoro wanakabiliwa na tatizo la kulala na maiti wodini kutokana na kituo hicho kutokuwa na chumba cha kuhifadhia maiti.

Hayo yamesemwa jana na daktari Mfawidhi wa kituo hicho Augustine Mnyamukama wakati akisoma risara ya watumishi kwa mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliyefika kituoni hapo kwa ajili ya kutoa vitanda vya kujifungulia viwili, vitanda vya kawaida vitano na mashuka kumi.

"Kama mgonjwa akifariki katika kituo chetu hakuna mahali pa kuhifadhia maiti jambo ambalo linawafanya wagonjwa wa wodi husika kulala na maiti hadi ndugu wa marehemu watakapokuja kuichukua maiti na kwenda kuizika", alisema.

Dk. Mnyamukama aliyataja matatizo mengine yanayoikabili kituo hicho kuwa ni upungufu wa watumishi, upungufu wa madawa muhimu pamoja na vifaa, vitanda vya kuzalishia na vya kawaida, hakuna wodi maalum ya akina mama wajawazito na wanaume, kutokuwepo kwa huduma ya upasuaji wa dharula , nyumba za watumishi, umeme na maji. Aliendelea kusema kuwa pamoja na matatizo hayo jitihada za pamoja zinafanyika kati ya wananchi na Serikali ili kuweza kutatua matatizo hayo.

"Hivi sasa tumefanikiwa kupata gari la kusafirisha wagonjwa wa dharula hali iliyosababisha kupungua kwa vifo wa watoto na kina mama wajawazito, tunatoa huduma ya Ugonjwa wa UKIMWI pia Halmashauri ya wilaya ya Bukoba kwa kushirikiana na wafadhili (JRF) wamewezesha kukarabatiwa kwa wodi ya watoto", alisema.

Aliyataja magonjwa yanayowasumbua wananchi wa eneo hilo kuwa ni maralia, magonjwa ya nayoshambulia mfumo wa hewa, kuharisha, minyoo, upungufu wa damu, vichomi na magonjwa yanayosababishwa na virusi vinavyosababisha Upungufu wa Kinga Mwilini.

Akikabidhi vifaa hivyo Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliwataka wananchi wa eneo hilo kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu kwa vizazi vijavyo. "Katika maeneo mengine wananchi wamekuwa wakiharibu na hata kuiba vifaa mbalimbali vinavyotolewa na wafadhili jambo ambalo limekuwa likikatisha tamaa na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi", alisema.

Kituo hicho kipo umbali wa kilomita 58 kutoka Hospitali ya mkoa kilijengwa mwaka 1947 kikiwa zahanati na ilipofika mwaka 1974 kilipandishwa hadhi na kuwa kituo cha Afya kinahudumia zaidi ya wakazi 13,574 pamoja na kuhudumia zahanati za Kishogo, Butainamwa, Kaibanja, Ruhunga, Kihumulo na Kyamulaile.

Kwa upande wa tiba kituo hicho kinatoa huduma ya wagonjwa wanaotibiwa nyumbani na kurudi (OPD), kutibu wagonjwa kwa wastaini 90 kwa siku na kulaza wagonjwa wa wastani kumi na tisa kwa siku. Pia kituo kinatoa huduma za kinga kwa mama na mtoto, uzazi wa mpango, elimu ya afya kwa jamii, huduma ya mkoba, kuzuia maambukizi ya Virusi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na upimaji wa virusi kwa hiari.

Mama Kikwete yuko katika ziara ya kikazi ya siku tatu katika mkoa wa Kagera yenye lengo la kuchangia juhudi za kupunguza vifo vya kinamama vinavyotokana na uzazi kwa kutoa vifaa vya huduma ya afya ya uzazi, hususan katika wodi za wazazi. Kuhamasisha juhudi za maendeleo kwa wanawake kupitia vikundi vya SACCOS na benki za vijijini- VICOBA.

Kuhamasisha juhudi za kupunguza matukio ya mimba na utoro mashuleni, kuhamasisha vikundi vya SACCOS na benki za vijijini- VICOBA na kuhamasisha juhudi za kupunguza matukio ya mimba na utoro mashuleni.

Msomaji
Kagera

2 comments:

Anonymous said...

Duu, ukiwa unaumwa wodini kugeuka unaona uliyekuwa unaongea naye kamaliza sijui inakuwaje?


Martin
Mwanza

Anonymous said...

Katerero wagonjwa wengi walishakufa kwahiyo swala la kifo kwao kawaida tu.

Masanja