Wednesday, November 18, 2009

OBAMA AWASILI KOREA KUSINI.

MIKATABA YA BIASHARA KATI YA MAREKANI NA KOREA KUSINI NDIO MAADA KUU


Rais Barack Obama wa Marekani amewasili Korea Kusini kituo cha mwisho cha ziara yake barani Asia ambapo suala la kuishawishi Korea Kaskazini kurudi katika mazungumzo ya kimataifa ya kutokomeza silaha za nuklea limatarajiwa kuhodhi mazungumzo kati yake na rais mwenzake wa Korea Kusini Lee Myung Bak.

Masuala mengine yatakayojadiliwa hapo kesho ni ushirika wa usalama pamoja na mkataba wa biashara huru uliokwama kati ya nchi hizo mbili.Serikali ya Korea Kusini imekuwa ikionyesha kuchoka kusubiri juhudi za serikali ya Marekani kuzungumzia upya sehemu za makubaliano makubwa ya Mkataba wa Biashara Huru (PTA) uliosainiwa takriban miezi 29 iliopita lakini bado ukisubiri kuridhiwa.

Msemaji wa Rais Lee wa Korea Kusini amesema wanatumai Rais Obama atatowa msimamo wa nguvu zaidi juu ya suala la mkataba huo na kwamba wanajiandaa kufanikisha hilo.
Taifa la kikomunisti la Korea Kaskazini limejaribu kuupima utawala wa Obama kwa kufyatua makombora kadhaa, kwa kufanya jaribio la pili la silaha za nuklea na vitendo kadhaa vya uhasama karibu na nchi rafiki wa Marekani Korea Kusini. Marekani imeweka wanajeshi wake 28,000 nchini Korea Kusini kuzima tishio lolote lile kutoka Korea Kaskazini na Obama anatazamiwa kuhutubia baadhi ya vikosi hivyo hapo kesho mchana kabla ya kuondoka kurudi Washington.


Manowari za Korea Kusini na Kaskazini zilishambuliana vikali kwa muda mfupi wiki iliopita baada ya Korea Kusini kusema kwamba mashua ya Korea Kaskazini ilivuka mpaka wa bahari wanaougombania.

Obama amesema serikali ya Marekani haiwezi kuoogopeshwa na vitisho vya nuklea vya Korea Kaskazini lakini iko tayari kuipatia nchi hiyo iliojitenga mustakbali wa usalama wenye ustawi na badala yake nchi hiyo ikubali kutokomeza kabisa silaha za nuklea.

Obama alisema 'Kwa miongo kadhaa Korea Kaskazini imeamua kufuata njia ya malumbano na uchokozi ikiwa ni pamoja na kutaka kuwa na silaha za nuklea .Kwa hiyo njia ya Korea Kaskazini kufanikisha mustakbali wake ni kurudi katika mazungumzo ya pande sita kutekeleza ahadi za nyuma ikiwa ni pamoja na kurudi katika mkataba wa kutokomneza silaha za nuklea na kutokomeza kabisa kunakoyakinishwa kwa silaha za nuklea katika bara la Korea.'

Tokea mwezi wa Augusti serikali ya Korea Kaskazini imekuwa ikitoa ishara ya kutaka amani kwa Marekani na Korea Kusini.Kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong- Il ameeleza kuwa tayari kurudi katika jukwaa la pande sita iwapo mazungumzo ya pande mbili kati yake na Marekani yanayotarajiwa mwezi ujao yatakuwa ya kuridhisha.

Rais Lee wa Korea Kusini amekuwa na ushirikiano wa karibu na Obama juu ya suala hilo na mengineyo lakini inatarajiwa kwamba Lee atamshinikiza mgeni wake huyo katika suala la makubaliano ya biashara huru ambayo yamekwama tokea yalipotiwa saini hapo mwezi wa Juni mwaka 2007.

Afisa wa rais wa Korea Kusini amekaririwa akisena wiki hii kwamba Rais Lee anatazamiwa kusisitiza umuhimu wa mkataba huo na kwamba ni zaidi ya miaka miwili tokea kusainiwa kakwe kwa hiyo unahitaji kuridhiwa haraka.

Wakati alipokuwa mgombea wa urais Obama aliutaja mkataba huo kuwa na kasoro kubwa sana na utawala wake tayari umedokeza kwamba unataka mabadiliko ya kuifunguwa zaidi Korea Kusini kwa wafanya biashara wa magari na nyama ya n'gombe wa Marekani.

Korea Kusini inapinga mazungumzo yoyote yale mapya kwa kile kitakachokuwa mkataba mkubwa kabisa wa biashara wa Marekani tokea ule mkataba wa biashara Huru wa Amerika Kaskazini wa mwaka 1994.

Obama hapo Jumatano alikamilisha ziara yake ya siku tatu nchini China ambapo amesema Marekani na China zinataka kutanuwa ushusiano wao wa kimkakati .

No comments: