Monday, November 16, 2009

KIKWETE AHUTUBIA MKUTANO WA USALAMA WA CHAKULA.

Rome, Italia

Ni jambo aibu kwamba bado watu wanaendelea kufa kwa njaa duniani, bila sababu ya maana, kwa sababu dunia inacho chakula cha kutosha kuweza kumulisha kila binadamu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema leo, Jumatatu, Novemba 16, 2009.

Akihutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi Kuhusu Hali ya Usalama wa Chakula Duniani katika makao makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) mjini hapa, Rais Kikwete amesema kuwa wakati umefika kwa dunia kukomesha aibu hiyo.

“Tokea nilipoanza kusoma hotuba yangu, kiasi cha sekunde 60 zilizopita, watoto kiasi cha kumi tayari wamekwishakufa kwa njaa. Ni dhahiri basi kuwa hatuna tena muda wa kupoteza katika kujaribu kukabiliana na balaa hili,” Rais Kikwete amewaambia wajumbe wa mkutano huo ulioanza leo asubuhi.

Rais Kikwete aliongeza, “Ni aibu kubwa kwa upande wetu kwa mtoto ama hata mtu mwingine yoyote mzima katika kona yoyote ya dunia yetu hii kwenda kitandani akiwa na njaa ama kufa kwa njaa. Kuna chakula cha kutosha kwenye ulimwengu wetu huu kuhakikisha kuwa vifo hivyo havitokei.”

Rais pia amesema kuwa dunia inazo nyenzo na raslimali za kutosha, teknolojia mwafaka na ujuzi unaofaa kuweza kuzalisha chakula cha kutosha kwa sasa na hata katika miaka ijayo. Amesema kuwa kinachotakiwa kwa dunia kutokomeza njaa duniani ni kwa kushirikiana na kuamsha ari muhimu ya kisiasa ili kuweza kukabiliana na changamoto hiyo.

“Kwa hakika ni jambo la kutia moyo kuwa Azimio la Mkutano huu tulilolipitisha asubuhi hii linathibitisha ari yetu ya pamoja kutaka kumaliza njaa wakati wa uhai wetu. Nimefurahi kuwa Azimio hilo limesisitiza umuhimu wa kurekebisha makosa ya kutokuwekeza kiasi cha kutosha katika “usalama wa chakula, kilimo na maendeleo.”

Rais Kikwete pia ametaka misaada ya maendeleo katika kilimo kuongezwa kwa kuwa imeshuka mno kutoka asilimia 19 mwaka 1980 hadi kufikia asilimia tano mwaka huu.“Sasa ni wakati wa kubadilisha hali hii. Ningependelea kuwa katika Azimio letu tungeweka malengo na muda wa kufikia malengo hayo, ama hata kulenga kuongeza maradufu kiwango hicho cha uwekezaji wa sasa katika kilimo.”

Rais Kikwete pia amezitaka nchi zinazoendelea kuhakikisha kuwa bajeti za nchi hizo zinakuwa na fedha za kutosha kulingana na misaada itakayotolewa na nchi tajiri ili kuwekeza katika kilimo.Akizungumzia kuhusu Tanzania amesema kuwa “kwetu sisi kilimo ni chakula na ni kila kitu katika maisha. Kiasi cha asilimia 80 ya watu wetu wote wanaishi vijijini na kilimo ndicho chimbuko lao kuu la maisha. Kilimo cha kisasa zaidi na chenye kuzalisha zaidi kitapunguza kiwango cha umasikini kidogo na kuongeza hali bora zaidi kwa watu wetu walio wengi.”

Rais Kikwete pia amesema kuwa uwekezaji katika kilimo utakuwa na athari kubwa na nzuri kwenye chumi za nchi masikini. “Wachumi wanabashiri, kwa imani kabisa, kuwa kila asilimia mia moja inayoongezeka kwenye uzalishaji wa kilimo, husababisha ongezeko la asilimia 1.6 ya nyongeza kwenye mapato ya asilimia 20 watu masikini zaidi katika kila nchi.”

Kuhusu uhusiano kati ya kilimo na tabianchi, Rais Kikwete amewaambia wajumbe wa Mkutano huo kuwa Tanzania ina matumaini makubwa kwamba Mkutano wa Tabianchi uliopangwa kufanyika mjini Copenhagen, Denmark, mwezi ujao, utafikia maamuzi muhimu yanayoweza kunufaisha kilimo na kubatilisha madhara ya tabianchi.“Wakati tunapokutana kwenye Mkutano Kuhusu Usalama wa Chakula, lazima tukumbuke kuwa ajenda ya usalama wa chakula haiwezi kamwe kutenganishwa na ajenda ya mazingira,”

Rais Kikwete aliongeza:“Kwa sababu ya madhara ya tabianchi, mienendo ya hali ya hewa imebadilika kabisa. Mvua hazitabiriki zaidi na hali ya ukame imekuwa mbaya zaidi na inayojitokeza zaidi. Hii imeathiri sana mazao, mifugo na usalama wa chakula kwa jumla. Mataifa yetu mengi na watu wake wanaotegemea kilimo sasa wamekuwa watu ambao maisha yao hayana uhakika na watu wa kutahayari zaidi.”

Rais Kikwete amekuwa miongoni mwa viongozi waliozungumza kwenye siku ya kwanza ya Mkutano huo wa siku tatu. Miongoni mwa viongozi wengine waliozungumza leo ni pamoja na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Benedict wa 16.

No comments: