Tuesday, March 10, 2009

SUDANI YAPIMA UWEZEKANO WA KUBADIRISHA WARANTI YA ICC

Sudan imesema,inachunguza iwapo waranti iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC kumkamata Rais Omar al-Bashir,itaweza kubatilishwa au kuahirishwa.
Hiyo ni ishara ya kwanza kuwa Sudan inashughulikia suala hilo. Hatua kama hiyo haimbatani kabisa na matamshi ya kejeli ya Rais Omar al-Bashir kupuuza waranti iliyotolewa na Mahakama ya Kiamatifa ya Uhalifu ikimtuhumu kuhusika na mauaji katika jimbo la Darfur, magharibi ya Sudan.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Ali Al-Sadig alipozungumza na shirika la habari la Reuters alisema,maafisa wa Sudan huenda wakalifikisha suala la waranti hiyo katika Mahakama ya Kimataifa ya Sheria na kuwaomba washirika wake washinikize kuiahirisha kesi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Amesema,majadiliano yanafanywa pamoja na China, Urusi na Libya-nchi wanachama katika Baraza la Usalama. Nchi hizo zimeshaeleza upinzani wake kuhusiana na waranti ya ICC.Sudan pia imearifiwa na Urusi na China kuwa mataifa ya magharibi yaliyosimama kidete kuipinga Khartoum pale waranti ya kumkamata Rais Bashir ilipokuwa ikitayarishwa,sasa huenda zikawa tayari kuijadili kesi hiyo.

Juma lililopita wanadiplomasia walisema,Uingereza,Ufaransa na Marekani, wote wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama,huenda wakaunga mkono pendekezo la kuiahirisha waranti hiyo,ikiwa maendeleo dhahiri yatapatikana huko Darfur na yatafanywa majadiliano thabiti ya amani.

Kwa maoni ya baadhi ya wachambuzi, serikali ya Sudan huenda ikahisi kuwa inatengwa pole pole kwani haikuungwa mkono hivyo na nchi za Mashariki ya Kati.Kwa upande mwingine wachambuzi wanasema,waranti hiyo huenda ikachochea machafuko zaidi katika jimbo la Darfur ambako vikosi vya amani vinajikuta katikati ya mgogoro huo.

Mahakama ya Kimataifa ya Sheria ni taasisi iliyo tofauti na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu,licha ya kuwa zote mbili zipo The Hague nchini Uholanzi.Kazi mojwapo kuu ya Mahakama ya Kimataifa ya Sheria ni kusuluhisha migogoro inayohusika na sheria.

Migogoro hiyo hufikishwa hupelekwa huko na wanachama wa Umoja wa Mataifa.Wataalamu wa kimataifa wanasema,si chini ya watu 200,000 wameuawa huko Darfur,wakati Khartoum ikisema ni watu 10,000 waliopoteza maisha yao.Mgogoro huo ulianza mwaka 2003 baada ya waasi,hasa wale wasio na asili ya Kiarabu waliposhika silaha kupambana na serikali ya Khartoum.

No comments: