Thursday, March 5, 2009

MZIGO MZITO WAIELEMEA HOSPITALI YA MKOA WA DODOMA.

Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ilijengwa mwaka 1930. Ilianza kama zahanati, ambapo baadaye ilipanuka na kuwa kituo cha afya na hatimaye hospitali. Kwa sasa ndiyo hospitali ya rufaa kwa wagonjwa kutoka wilaya sita za Mkoa wa Dodoma, ambazo ni Bahi, Chamwino, Dodoma Mjini, Kondoa, Kongwa na Mpwapwa. Licha ya hospitali hiyo kuwa ya rufaa, pia inahudumia wakazi wote wa Mkoa wa Dodoma, wanaokisiwa kuwa ni zaidi ya milioni mbili.

Watu wanaohudumiwa katika hospitali hiyo ni wengi, ikilinganishwa na wafanyakazi 400 waliopo na vitanda 420 vilivyopo hospitalini hapo.Pamoja na kuwapo hospitali kuu ya mkoa, mkoa wa Dodoma una vituo vya kutolea huduma za afya. Kuna jumla ya hospitali saba, ambapo tano ni za serikali na mbili ni za watu binafsi.

Kuna jumla ya vituo 25 vya afya, ambapo 20 ni vya serikali na vitano vya watu binafsi. Kuna zahanati 277, ambapo 220 ni za serikali na 57 za watu binafsi. Pamoja na kuwapo kwa vituo vingi vya afya, bado hospitali ya Mkoa wa Dodoma imekuwa ikihudumia idadi kubwa ya watu, hususan wakati wa vikao vya Bunge, ambapo Mji wa Dodoma hukusanya watu wanaofikia 400 kila siku.

Licha ya vikao vya Bunge, pia hospitali hii hupokea wagonjwa wa kawaida wanaohitaji huduma kutoka mikoa mbalimbali, kutokana na mazingira ya kijiografia.Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Geodfrey Mtey, anasema kwa siku hospitali yake hupokea wagonjwa wa nje kati ya 300 hadi 500 na pia huwa na wagonjwa waliolazwa kati ya 300 na 500.

Dk. Mtey anasema kuwa kwa mwaka wagonjwa 31,515 hulazwa, ambapo wastani wa mgonjwa kukaa hospitalini ni siku nne hadi siku tano. Mganga Mkuu huyo anasema kuwa lengo kuu ni kuwapo kwa huduma za afya za ngazi ya rufaa, zitakazokidhi mahitaji makubwa ya huduma za tiba na kinga katika Mkoa wa Dodoma.

Anasema mahitaji yanaongezeka, kutokana na kasi iliyopo ya kuhamia Dodoma na kuanzishwa kwa taasisi za kijamii, ikiwamo vyuo vikuu vipya, ambavyo ni Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kinachomilikiwa na Serikali na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana, kinachomilikiwa na Kanisa Anglikana.

Anasema kuna mpango wa kuifanya hospitali hiyo, kuwa na uwezo wa kutoa huduma maalumu na za daraja stahiki za kutosheleza mahitaji ya taasisi, zitakazokuwa na wafanyakazi wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na bima nyingine.“Viongozi wa kitaifa wakiwamo wabunge, kwa kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano linafanya vikao vyake kwa muda usiopungua miezi sita hapa Dodoma, wataandaliwa pia huduma zao,” anasema Dk. Mtey.

Aidha, Mganga Mkuu huyo anasema lengo lingine ni kuifanya hospitali hiyo, kuwa ni kitovu cha kufundishia kwa vitendo wataalamu mbalimbali wa afya, ikiwa ni pamoja na wataalamu wa ngazi za chini wanaohitajika kwa wingi katika kufanikisha Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM).

Dk. Mtey anasema kuwa ili malengo hayo yafikiwe ni lazima kuboresha hali ya utumishi na watumishi, kufikia kiwango stahili kitaaluma na kiikama ifikapo mwaka 2015 na kuongeza eneo la kuboresha hali ya miundombinu ya hospitali kukidhi mahitaji ya hospitali ya ngazi ya rufaa ifikapo mwaka huo.

Anataja mkakati mwingine kuwa ni ule wa kuboresha upatikanaji wa vifaa vya tiba na dawa kwa ngazi ya hospitali ya rufaa ifikapo mwaka 2015 na kuwapo kwa mifumo na huduma saidizi za msingi zenye kukidhi viwango vya hospitali ya rufaa.

Pamoja na kuwapo kwa mipango hiyo ya kuhakikisha hospitali hiyo inakuwa katika ngazi ya rufaa, Dk. Mtey anataja changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili hospitali hiyo kuwa ni upungufu wa watumishi, kulinganisha ikama na mahitaji na kuwapo kwa baadhi ya watumishi wachache waliokata tamaa na wazembe.

Changamoto nyingine ni wingi wa wagonjwa unaotokana pamoja na mambo mengine kutokuwapo utaratibu mzuri wa mfumo wa rufaa na upungufu wa maeneo ya kutosha kwa ajili ya upanuzi.

Changamoto nyingine ni miundombinu ya majengo, barabara, umeme, maji na mawasiliano isiyokidhi viwango vya utoaji huduma bora na mahitaji ya wagonjwa waliopo. Pia, Dk. Mtey anasema kuna upungufu wa vifaa vya tiba na dawa za kutosha kwa wakati wote na ufinyu wa bajeti.

Anasema mikakati mbalimbali ya kukabiliana nazo, imewekwa ambayo ni pamoja na kuongeza watumishi wa kada mbalimbali kulingana na ikama; na kuinua ari na moyo wa watumishi kufanya kazi. Mkakati mwingine ni kupeleka maombi serikalini ili kupatiwa eneo la kutosha, kwa ajili ya kujenga majengo mapya. Mkakati mwingine ni kukarabati majengo ya sasa na kuongeza samani na dawa.

Dk. Mtey anasema ili kuhakikisha hayo yanafanyika, tayari majengo mapya yameanza kujengwa, ikiwemo jengo la ghorofa moja la wagonjwa wa nje (OPD), ambalo litakuwa na sehemu za kuhudumia wagonjwa wa kawaida na wa dharura, sehemu ya kupumzikia wagonjwa kawaida na sehemu za ofisi za kliniki za ushauri nasaha na upimaji magonjwa maalumu, kama macho, ngozi, meno, pua, masikio, koo na kifua kikuu.

Pia, jengo hilo litakuwa na sehemu za maabara ndogo, ofisi za viongozi, waganga na wauguzi wa hospitali, sehemu ya X-ray, sehemu ya mazoezi ya viungo na sehemu ya maduka na mgahawa.

Dk. Mtey anasema pia kuwa jengo la wazazi la ghorofa moja, limeanza kujengwa na pia jengo la grade 1 litajengwa kwa mkopo kutoka Bima ya Afya. Baadhi ya majengo yatabomolewa, likiwamo jengo la maabara la zamani.

Hivi sasa hospitali hiyo imepata jengo jipya la maabara, lililojengwa na Shirika la Ujerumani la ABBOTT kwa dola za Marekani 389,000. Upanuzi huo utawezesha hospitali hiyo, kuwa na uwezo wa kupokea wagonjwa wa nje 500 hadi 600 kwa siku, zikiwamo huduma maalumu.

“Upanuzi huu utawezesha hospitali kuwa na vitanda 740 kutoka vitanda 420 vilivyopo sasa na kuhudumia madaktari na wauguzi wanafunzi, watakaokuwa katika mazoezi ya vitendo 30 hadi 50 kwa wakati mmoja,” anasisitiza.

Martha Mtangoo.
Dodoma.

No comments: