Monday, March 2, 2009

HOTUBA YA MWISHO WA MWEZI YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI TAREHE 28 FEBRUARI, 2009

Utangulizi

Ndugu Wananchi;
Naomba tuendelee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia tena fursa nyingine ya kuzungumza kuhusu masuala muhimu ya nchi yetu katika siku hii ya mwisho ya mwezi Februari 2009. Leo nakusudia kuzungumzia mambo manne, nayo ni:
(a) Mapokezi ya wageni wetu kutoka nchi za nje;
(b) Hali ya chakula nchini;
(c) Ukatili dhidi ya walemavu wa ngozi (Albino); na
(d) Malimbikizo ya madai ya Watumishi wa umma.

Mapokezi ya Wageni Wetu Kutoka Nchi za Nje

Ndugu Wananchi;
Mwezi huu tunaoumaliza leo ulikuwa na baraka tele kwa nchi yetu. Tumepata bahati ya kutembelewa na wageni mashuhuri watano kutoka nchi za nje. Wa kwanza alikuwa Rais Rupia Banda wa Zambia aliyetutembelea tarehe 9 mpaka 10 Februari, 2009. Wa pili alikuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Hu Jintao aliyetutembelea tarehe 14 mpaka 16 Februari. Akafuatiwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Mhe. Kamalesh Sharma tarehe 20, Februari. Tarehe 22 hadi 23 Februari, tulikuwa na ugeni wa Rais wa Uturuki Mheshimiwa Abdullah Gül. Hatimaye tarehe 26 Februari, tukawa na ugeni wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki-moon ambaye ameondoka nchini leo.

Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru sana wananchi wenzangu hasa wa hapa Dar es Salaam na maeneo mengine walikotembelea wageni wetu kwa mapokezi mazuri. Tumewapokea kwa upendo mkubwa na wote wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri za nchi yetu na ukarimu wa watu wake. Mmeturahisishia sana kazi yetu ya kujenga mahusiano mema na nchi hizo na mashirika hayo muhimu ya kimataifa.

Viongozi hao tumefanya nao mazungumzo mazuri ambayo yamelenga kukuza ushirikiano baina ya nchi yetu na nchi zao pamoja na mashirika wanayoyaongoza. Mazungumzo yetu yalikuwa ya mafanikio tuliyoyatarajia. Kilichobaki kwa upande wetu na wao ni kufuatilia utekelezaji wa yale tuliyokubaliana. Kwa upande wetu tumejipanga vizuri kufanya hivyo na wenzetu pia wamenihakikishia kufanya hivyo. Baadhi wamekwishaanza utekelezaji.

Kwa mfano, Gavana wa Benki ya Maendeleo ya China anakuja nchini mwishoni mwa wiki kwa mazungumzo na Gavana wa Benki Kuu kuhusu maombi yangu kwa Rais Hu Jintao ya kutaka serikali zetu zishirikiane kuongeza mtaji wa Benki ya Rasilimali (TIB) na kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo.

Ndugu Wananchi;
Mwezi ujao wa Machi, nchi yetu imepewa heshima nyingine kubwa ya kimataifa. Kwa makubaliano baina yangu na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa yaani IMF, Bw. Dominique Strauss-Khan, Tanzania tutakuwa mwenyeji wa mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu wa nchi za Afrika na IMF. Mkutano huo tunaouitisha kwa pamoja utafanyika hapa Dar es Salaam tarehe 10 na 11 Machi, 2009.Agenda kuu ya mkutano ni Hali ya Uchumi wa Dunia ilivyo sasa na athari zake kwa nchi za Afrika. Lengo ni kutafakari hali ya machafuko ya mfumo wa fedha wa kimataifa na kudhoofika kwa uchumi wa mataifa makubwa kiuchumi duniani na jinsi matatizo hayo yanavyoathiri na kutishia ustawi wa uchumi wa watu katika bara la Afrika.

Jambo la msingi katika mkutano huo ni kuelewana kwa pamoja kuhusu mikakati na mbinu za kukabiliana na tishio hili kubwa kuliko yote kutokea duniani tangu miaka ya 1930.
Nawaomba Watanzania wenzangu kama ilivyo kawaida tuwapokee wageni wetu hao nao kwa mujibu wa takrima na upendo wa asili wa wananchi wa nchi yetu. Mambo ambayo yametuletea sifa na heshima kubwa duniani na kutufanya tuwe na marafiki wengi.

Ndugu Wananchi;
Wakati sisi tukiwa wenyeji wa mkutano wa Mawaziri wa Fedha wa Afrika na IMF, mjini London,
Uingereza kutakuwa na mkutano wa uwekezaji wa Afrika Mashariki. Nchi zote tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zitashiriki. Rais wa Zanzibar Mhe. Amani Abeid Karume ataongoza ujumbe wa Tanzania. Mkutano huu unaoandaliwa na marafiki zetu wa jiji la London ni fursa nzuri ya kutangaza vivutio vya uwekezaji vya nchi yetu. Tumejiandaa vya kutosha. Naamini wenzetu wanaotuwakilisha watashiriki vizuri.

Hali ya Chakula Nchini

Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwaka 2008 nilieleza kuwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini imekuwa nzuri kwa miaka miwili mfululizo, yaani 2007 na 2008, tofauti na ilivyokuwa mwaka 2006. Nilieleza pia hofu yangu kuwa kutokana na kukosekana kwa mvua za vuli katika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, hali ya upatikanaji wa chakula katika mikoa hiyo inaweza kuwa ya matatizo siku za usoni.

Na, inaweza kuwa mbaya zaidi kama mvua za masika nazo hazitanyesha vizuri.Baadae katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Januari, 2009 nilielezea mashaka yangu kuwa katika baadhi ya mikoa inayopata mvua moja kwa mwaka, nako kumejitokeza uhaba mkubwa wa mvua. Nilieleza pia wakati ule kuwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inafanya tathmini ya hali ya chakula nchini na watatoa taarifa yao ipasavyo baada ya kazi hiyo kukamilika.
Kazi hiyo imekamilika na taarifa imetolewa na inaendelea kufanyiwa kazi.

Ndugu Wananchi;
Mvua za msimu katika mikoa inayopata mvua mara moja kwa mwaka (Mikoa ya Kati, Magharibi, Nyanda za Juu Kusini Magharibi na Kusini) zinaendelea kunyesha kwa viwango vya wastani na chini ya wastani katika maeneo mengi. Mikoa ya Lindi na Mtwara kati ya mwezi Desemba, 2008 na Januari, 2009 ilikabiliwa na vipindi virefu vya ukame uliosababisha karibu asilimia 90 ya mazao ya chakula yaliyopandwa mwanzoni mwa msimu kunyauka.

Hata hivyo, mvua sasa zinaendelea kunyesha. Serikali imetoa msaada wa mbegu na wakulima ambao wamelazimika kupanda tena. Tuendelee kumuomba Mungu mvua ziendelee kunyesha ili jaribio hili la kupanda mara ya pili liwe na matokeo tunayoyatarajia.

Ndugu Wananchi;
Kwa jinsi hali ya mvua ilivyo nchini, ni dhahiri kuwa mavuno ya msimu ujao huenda yakawa pungufu.
Labda mvua za masika ziwe nzuri sana na mvua zinazoendelea sasa katika mikoa iliyoathirika ziendelee kunyesha vizuri mpaka mwisho wa msimu.Upatikanaji wa ChakulaNdugu Wananchi;Tathmini ya hali ya chakula nchini iliyofanywa na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inaonesha kuwa hadi kufikia mwezi Desemba, 2008 mavuno ya mazao ya chakula yalifikia jumla ya tani milioni 10.872 wakati makadirio ya mahitaji nchini ni tani milioni 10.337.

Kuna ziada ndogo ya tani 535,000. Ziada hii ni ndogo mno. Haiweze kuleta utulivu wa kutosha kwa upande wa upatikanaji wa chakula kwa msimu unaoishia Juni, 2009. Hivyo, kuhitajika tahadhari na uangalifu mkubwa katika hifadhi na matumizi ya chakula. Hili ni muhimu sana hasa ikizingatiwa kwamba ziada hii inatokana na mazao ya chakula yasiyo ya nafaka kama vile muhogo, ndizi, viazi na mazao ya jamii ya kunde.

Tathmini hiyo imebainisha kuwepo kwa upungufu wa chakula katika wilaya 19 nchini. Tani 7,128 zimetengwa kusaidia watu katika wilaya hizo. Mpaka Februari 25, 2009 tani 3,265 zilikuwa zimeshagawiwa kwa watu katika wilaya hizo. Kati ya hizo tani 359 zilitolewa bure kwa watu 12,027 wasiokuwa na uwezo wa kununua.Mwenendo wa Bei za Vyakula Nchini.

Ndugu Wananchi;
Tathmini ya hali ya chakula nchini, pia, imeonesha kuwa bei za vyakula nchini zimeendelea kupanda. Zipo sababu kadhaa na mojawapo kubwa ni ile ya kutokuwepo ziada kwa mazao ya mahindi na mchele ambavyo ndivyo vyakula vikuu. Pia, hali ya upungufu mkubwa wa chakula katika nchi jirani ambazo zimetokea kutegemea Tanzania kupata mahitaji yao ya chakula, imekuwa kichocheo kikubwa cha kupanda kwa bei za ndani za chakula hapa nchini.

Wenzetu wako tayari kununua chakula chetu kwa bei yoyote ile jambo ambalo limetumika na wauzaji nchini kama kigezo kwa bei wanazouzia mahindi na mchele hapa ndani.Wakati mwingine matatizo ya miundombinu nayo yamechangia kupanda kwa bei za vyakula katika baadhi ya maeneo hapa nchini. Kwa mfano, katika mwezi Januari 2009, soko la Lindi liliongoza kwa kuwa na bei ya juu zaidi ya mahindi iliyofikia Shs.45,000/= kwa gunia wakati soko la Sumbawanga lilikuwa na bei ya chini zaidi ya Shs.26,455/= .

Kama kungekuwa na njia rahisi ya kufikisha mahindi ya Rukwa mkoani Lindi bei isingekuwa juu kiasi hicho.Hali ya Hifadhi ya Chakula Nchini na Hatua za Serikali

Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kwa mara nyingine tena kuwa, Serikali yetu inafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa hayupo mwananchi yeyote atakayekufa kwa njaa.
akiba ya kutosha ya chakula katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA). Hadi tarehe 25 Februari 2009, akiba ya chakula iliyohifadhiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ilikuwa tani 125,673 za nafaka. Wakati huohuo, hadi tarehe 31 Januari, 2009 wafanyabiashara wakubwa wa mazao ya chakula nchini walikuwa na akiba ya jumla ya tani 149,200 za mazao ya nafaka zikiwemo tani 38,608 za mahindi, tani 1,637 za mchele, tani 107,870 za ngano na tani 1,090 za mtama.Tuko tayari wakati wowote kuitumia akiba yetu hiyo kuokoa maisha ya Watanzania pale itakapohitajika kufanya hivyo.

Tunafanya hivyo hivi sasa katika baadhi ya maeneo kama nilivyokwishaeleza. Aidha, tuko tayari kutumia akiba hiyo kupunguza makali ya bei za vyakula nchini. Tunajiandaa kufanya hivyo baada ya muda mrefu kwa upande wa mchele.Wito wa Serikali kwa Wananchi

Ndugu Wananchi;
Tishio la upungufu wa chakula ni jambo la hatari ambalo sote, Serikali na wananchi, hatuna budi kulichukulia kwa uzito unaostahili. Nimeeleza jinsi Serikali tulivyojipanga kutimiza wajibu wetu.
Napenda kuitumia nafasi hii kusisitiza au kutoa wito kwa wananchi nao kutimiza wajibu wao.Tunawategemea kuzingatia mambo matatu yafuatayo:

Kwanza,
tutumie vizuri akiba ya chakula tuliyonayo. Tulitambue tishio lililopo na kuwa waangalifu, hali siyo nzuri sana, inaweza kuwa mbaya mbele ya safari. Tuwe na tahadhari kubwa. Kwa sababu, hali ya upungufu wa chakula ilivyo duniani hivi sasa, tunaweza kuwa na fedha lakini tukakosa chakula cha kununua.

Pili,
maeneo yaliyopata tatizo la upungufu wa mvua wazitumie mvua zinazonesha sasa kupanda mazao yanayostahimili ukame na hasa yale yenye kukomaa kwa muda mfupi.

Tatu,
tuongeze bidii kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula ili tujitosheleze kwa chakula na kuuza akiba nje ya nchi. Tuzingatie kanuni za kilimo bora na tutumie pembejeo za kisasa.

Tunawasihi wanaopata mvua za masika wahakikishe kuwa wanazitumia vizuri ili kufidia pengo la upungufu. Serikali kupitia Mfuko wa Maafa ilitoa tani 1,091 zenye thamani ya shilingi bilioni 1.76 kwa ajili ya wakulima waliolazimika kupanda tena baada ya mazao yao kunyauka. Tuko tayari kutoa ziada kama hapana budi.

Mauaji ya Albino

Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwaka jana tarehe 31 Desemba 2008, nilitamka juu ya uamuzi wangu wa kuitisha na kuendesha zoezi la Kura ya Maoni nchi nzima kuhusu mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, yaani Albino. Dhamira yangu ni kuwapa nafasi wananchi ya kuwataja watu wanaowafahamu kuwa wanajihusisha na mauaji ya albino au kukata viungo vyao.

Pia wawataje watu wanaojihusisha na biashara ya viungo vya albino na watumiaji wa viungo hivyo. Kadhalika, wananchi wasaidie kuwataja waganga wa jadi wanaojihusisha na upigaji ramli au uganga unaohitaji matumizi ya viungo vya albino. Aidha, watu wawataje wanaojihusisha kwa namna yoyote ile na jambo lolote linalosababisha mauaji ya Albino.

Ndugu Wananchi;
Maandalizi ya kutekeleza uamuzi wangu huo yanaelekea kukamilika. Mheshimiwa Waziri Mkuu atafanya uzinduzi rasmi wa zoezi hilo mwishoni mwa wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2009 na zoezi lenyewe la kupiga kura kufanyika kuanzia wiki ya pili ya Machi, 2009. Katika zoezi hilo pia wauaji wa vikongwe, majambazi wa kutumia silaha na wauzaji wa madawa ya kulevya nao watahusishwa.Katika kuendesha zoezi hili, Mikoa imegawanywa katika Kanda saba zifuatazo:

Kanda ya Ziwa inayojumuisha Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, na Shinyanga; Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye Mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma; Kanda ya Kati ya Mikoa ya Dodoma, na Singida; Kanda ya Kusini yenye Mikoa ya Lindi na Mtwara; Kanda ya Magharibi yenye Mikoa ya Kigoma na Tabora; Kanda ya Kaskazini yenye kujumuisha Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara; na Kanda ya Mashariki itakayokuwa na Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Wakuu wa Mikoa yote Nchini wameshapewa Mwongozo wa jinsi ya kutekeleza zoezi hili. Miongoni mwa mambo ya kuzingatia ni haya yafuatayo:
(a) Kuelimisha na kuhamasisha wananchi kushriki katika zoezi hili. Kazi hiyo inaendelea.
(b) Kwamba Upigaji Kura ufanyike mwezi Machi, 2009 kwa tarehe zitakazopangwa kwa kuzingatia Kanda nilizokwisha kuzitaja. Kila Kanda itachagua siku yake maalum ya kuendesha kura hizo. Kanda ya Ziwa itakuwa ya kwanza.

(c) Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa zikiongozwa na Wakuu wa Mikoa zisimamie zoezi hili kwa makini. Kadhalika, Kamati za Ulinzi na Usalama za wilaya zikiongozwa na Wakuu wa Wilaya zitaongoza utekelezaji katika Wilaya zao na kushirikisha serikali za vijiji na mitaa.Aidha, Serikali imewaagiza Wakuu wa Mikoa kuzingatia mazingira ya kila Kanda ili waweze kutumia utaratibu wowote utakaoonekana kufaa kuleta ufanisi wa hali ya juu katika kutimiza dhamira ya Kura hizi za Maoni.

Ndugu Wananchi;
Napenda kuitumia fursa hii kuwasihi Watanzania, wake kwa waume, vijana na wazee tujitokeze kwa wingi kuwataja watu wanaojihusisha na maovu hayo katika jamii. Kura ni siri, hakuna atakayejua umemtaja nani. Hata msimamizi wa kituo hawezi kujua. Naomba tusaidiane tukomeshe ukatili huu na aibu hii katika taifa letu. Jina la nchi yetu limechafuliwa sana kwa vitendo vya watu wachache waovu waliotawaliwa na tama ya utajiri iliyopita mipaka. Inawezekana, timiza Wajibu Wako!!

Malimbikizo ya Madai ya Watumishi Serikalini

Ndugu Wananchi;
Hivi karibuni nilipokutana na viongozi wa kisiasa na kiutendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nilizungumzia malimbikizo ya madai ya malipo ya stahili mbalimbali za walimu. Jambo hilo limekuwa chanzo cha mivutano kati ya Serikali na walimu. Katika mazungumzo yangu nao, nilisisitiza kuwa mivutano hiyo haina lazima wala sababu ya kuwepo.

Kama wahusika katika idara za utawala na fedha katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Utumishi na Wizara ya Fedha na Uchumi wangetimiza ipasavyo wajibu wao hakuna tatizo. Napenda kusema kuwa matatizo wayapatayo walimu ndiyo wayapatayo watumishi wengine wa umma katika Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali.Sehemu kubwa ya madai ya malimbikizo ya walimu yanahusu stahili zao za uhamisho, kupandishwa madaraja, likizo n.k.

Nilielekeza kuwa kama Halmashauri haina pesa za uhamisho wasiwahamishe watumishi wao. Wamekuwa wanafanya hivyo na kulimbikiza madeni makubwa ambayo yamekuwa yanalipwa na Serikali Kuu mara nyingi baada ya walimu kuchachamaa. Serikali Kuu imekuwa inafanya hivyo kuepusha shari, bahati mbaya hiyo imegeuka kuwa mazoea. Sasa inaonekana kana kwamba kumhamisha mtumishi kutoka kituo kimoja kwenda kingine Wilayani ni wajibu wa Serikali Kuu kugharamia. Matokeo yake ni malimbikizo na madai yasiyokwisha yanayozua migogoro ya mara kwa mara.

Baya zaidi panapotokea migogoro hiyo wale waliosababisha malimbikizo hayo hawaonekani kuwa ndiyo wakosaji bali inaonekana Serikali Kuu ambayo huingilia kati kuokoa jahazi. Hali hii haiwezi kuachwa iendelee.

Ndugu Wananchi;
Niliagiza mtindo wa kuhamisha walimu bila ya kuwa na fedha za uhamisho ukomeshwe mara moja. Ni marufuku kufanya hivyo. Na, agizo langu hilo haliwahusu walimu tu, bali watumishi wote wa umma. Kiongozi au mhusika yeyote atakayekiuka agizo hili alipishwe yeye gharama za kumhamisha mtumishi huyo.Madai ya likizo nayo yako kama ya uhamisho.

Ninachosema kama hazikutengwa fedha za kugharamia likizo za watumishi, usilimbikize madeni. Uzuri wa likizo ni kuwa hazipotei. Wakati wa kustaafu siku za likizo ambazo mtumishi hakuchukua hulipwa. Hata hivyo, napenda kusisitiza kutengwa fedha za kutosha za likizo kwani mapumziko ni muhimu kwa wafanyakazi.

Ndugu wananchi;
Tulikubaliana pia kwamba suala la kuwapandisha watumishi vyeo bila kuwarekebishia mishahara yao ni upungufu wa kiutendaji ambao ni lazima ukomeshwe mara moja.

Nimeagiza viongozi wa Wizara zote na Halmashauri kuhakikisha kuwa watumishi wote wanaopandishwa vyeo wanalipwa stahili zao kwa wakati. Napata ugumu kuelewa kwanini kuwepo tatizo hili. Hivi inatokeaje mtumishi wa umma apandishwe ngazi au cheo na kuwa na tatizo la kumlipa mshahara wa ngazi mpya kwa mwaka au miaka? Nina ushahidi wa mwalimu kupandishwa madaraja mara tatu lakini bado analipwa mshahara ule ule wa kabla hajapandishwa daraja la mwanzo.

Hii si sawa hata kidogo na siyo haki.Kwa mujibu wa utaratibu wa Serikali, mtumishi hupandishwa cheo kwa misingi miwili.
Kwanza,
kutimiza masharti ya muundo wake wa utumishi, na pili, kuwepo kwa fedha kwenye bajeti ya Wizara au Idara husika kwa madhumuni hayo. Je, iweje leo mtu apandishwe madaraja bila kulipwa mashahara stahiki? Hili halikubaliki. Nimewataka wahusika warekebishe kasoro hii ambayo haina sababu ya kuwepo. Ni migogoro ya kujitakia, Kwa nini tuwe watawala wa aina hii kwa watumishi tunaowaongoza?

Ndugu Wananchi;
Mlundikano wa malimbikizo ya madai ya watumishi husababishwa na wakuu wa kazi wazembe na wasiojali maslahi ya walio chini yao. Aghalabu, unasababishwa na watumishi wa Idara ya Fedha na Utumishi wasio waaminifu ambao wamekuwa wakijinufaisha kupitia mlundikano wa madai ya watumishi. Nimeagiza Viongozi wa Wizara ya Elimu kuwashughulikia ipasavyo watumishi wa aina hiyo wasichelee kuwaondoka kwenye nafasi zao.

Wakati mwingine watu kukaa kituo kimoja kwa muda mrefu huzaa tabia za namna hii. Nimeagiza watu walioko kituo kimoja kwa muda mrefu wahamishwe. Kuwahamisha mara kwa mara kutasaidia kuondoa usultani.

Ndugu Wananchi,
Naomba nimalize kwa kuwashukuru kwa kunisikiliza. Tuendelee kushikamana kujenga nchi yetu. Lakini pia kwa pamoja tuwapongeze wachezaji wetu wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa ushindi walioupata majuzi na tuzidi kuwahamasisha washinde pia mchezo wao wa leo na mingine inayofuata. Tuelekeze dua zetu kwao.

Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Asanteni Sana

2 comments:

Anonymous said...

Thanks ccm marekani for the best information.

Anonymous said...

jk nafurai jinsi unavyoendsha nchi yetu, kuruhusu vyombo vya habari kutufikishia taharifa ote popote pale tulipo, sio mambo ya kuficha ficha.

Nawapongezeni ccm kwa tovuti hii