Tuesday, December 1, 2009

Wanafunzi wa shule za sekondari watakiwa kuzijua haki zao za msingi!!

Makamu Mwenyekiti wa tume ya haki za binadamu na utawala Bora Mahfoudha Alley Hamid katika moja ya mikutano aliyowahi kuifanya na waandishi wa habari.

Wanafunzi wa shule za Sekondari hapa nchini wametakiwa kuzijua haki zao za msingi ambazo zitawasaidia kupata mahitaji yao ya muhimu bila ya kunyanyaswa na watu wachache ambao hawapendi kuzifuata haki za binadamu na utawala bora.

Wito huo umetolewa jana na Mary Massay ambaye ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya haki za Binadamu na Utawala bora wakati wa mdahalo wa wananafunzi wa shule za sekondari kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kuhusu haki za binadamu uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa tume hiyo uliopo jijini Dar es Salaam.

Massay alisema kuwa ofisi za tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora imekuwa ikichapisha vitabu, majarida na vipeperushi mbalimbali vinavyoelezea haki za binadamu katika makundi mbalimbali hivyo basi kama wanafunzi hao watakuwa na bidii ya kusoma machapisho hayo yatawasaidia kujua haki zao.

Alisema, "Hivi sasa tume ya haki za binadamu na utawala bora imeamua kutokuwaacha nyuma watoto kwani nao ni wanajamii na ni sehemu ya haki za binadamu hivyo basi inawafundisha mambo ya muhimu kuhusiana na haki za binadamu ili nao watakaposhika madaraka hapo baadaye wajue la kufanya".

Aliendelea kusema kuwa wananchi wengi katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa na uelewa mkubwa kuhusu haki za binadamu na utawala bora jambo la muhimu lililopo ni kuzilinda na kuzitetea haki hizo."Ni jukumu la watanzania wote kujua haki za binadamu ni zipi kwani katika maisha tunayoishi kila siku haki za binadamu zipo.

Kwa mfano unaweza kujiuliza Je shuleni watoto wanapewa nafasi ya kuchangia? Wazazi wanawashirikisha watoto wao katika mambo mbalimbali ya familia?, kama hakuna ushirikishwaji wa watoto basi haki za binadamu hazifuatwi hapo", alisema Massay.

Msomaji
Dar es salaam

No comments: