Benjamin SaweMaelezo Dar es Salaam .Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini imesema wakala wa ukusanyaji madeni sugu kampuni ya Majembe Auction Mart inafanyakazi chini ya Sheria ya utekelezaji wa masharti ya leseni za usafirishaji ya mwaka 2007.
Meneja wa Ufundi na Usalama wa SUMATRA Aron Kisaka alisema wameichagua Majembe Auction Mart ili kuimarisha usimamizi wa utoaji huduma za usafiri Dar es Salaam na kuwataka madereva wa daladala kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo
Bwana Kisaka alisema hayo hivi karibuni katika mkutano uliondaliwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Said Mwema uliokuwa na lengo la kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta ya usafiri nchini.
Aidha wadau na wananchi kwa ujumla wanaombwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka zinazosimamia usafiri pamoja na Kampuni ya Majembe kwa lengo la kuimarisha usimamizi na kuboresha huduma hii muhimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam .
Bwana Kisaka alisema Majembe kazi yao ni kufuatilia utekelezaji wa masharti ya leseni ya usafirishaji abiria na si utozaji wa faini ambapo kazi ya utozaji wa faini hufanywa na SUMATRA .
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Said Mwema alisema utendaji wa kazi wa Majembe ni wa kitaalamu kwani Jeshi la Polisi liliwapa semina ya siku moja juu ya utendaji kazi na linaendelea kuwafunza zaidi kwa vitendo
Pia Bwana Mwema alisema Jeshi la Polisi limejiandaa vema katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka katika sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na nchi kavu,hewani,majini,na mipakani katika kulinda usalama na amani nchini.
Kampuni ya Majembe Auction Mart ambayo imeteuliwa kufanya kazi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja itatekeleza majukumu waliyopewa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani.
Msomaji
Dar es salaam
No comments:
Post a Comment