Wednesday, December 2, 2009

Katibu mkuu wa CCM Mhe Yusufu Makamba akazia wito wa harambee ya uchaguzi wa CCM

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, ndugu Yussuf Makamba (Mb) ametoa ufafanuzi wa Kauli ya Katibu wa NEC Uchumi na Fedha, ndugu Amos Makala kutokana na habari iliyochapishwa na gazeti la Majira la Desemba Mosi, 2009 lenye Kichwa cha habari “Kauli ya fedha za kampeni moto CCM”.

Makamba alisema hapingani na Mkakati sahihi wa Idara ya Uchumi na Fedha wenye nia nzuri ya kukipatia Chama fedha kwa njia ya uwazi usiotia shaka yoyote. Kwa kuhofia mwandishi kupotosha jambo kubwa kama hili alimtaka awasiliane na Makala mwenyewe ili aweze kupatiwa ufafanuzi wa kina kwani ndiye Mkuu wa Idara mwenye Mamlaka ya kuelezea mipango na mikakati yote iliyo chini yake.

Alisema mwakani tuna uchaguzi mkuu wa Dola, moja ya kazi ya idara yake ni kubuni mikakati na mbinu halali za kukitafutia Chama fedha, ikiwa ni katika kutekeleza awamu ya tatu ya mradi wa kuimarisha Chama.

Mbinu hizo ni pamoja na kila mwanachama, wapenzi na wakereketwa wa CCM wanatakiwa kukichangia Chama, kuanzisha harambee katika ngazi zote za chama ili kutunisha mifuko ya uchaguzi katika ngazi hizo na kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kupitia ujumbe mfupi (SMS) . Huo ni utaratibu wa kawaida ambao hutumiwa pia na taasisi za mbali mbali.

Makamba anasema Mpango huo wa Idara umetangazwa huko Ruvuma, na Kibaha na Mkuu wa Idara mwenyewe, anawaomba watu wenye mapenzi mema na CCM walione hili kwamba ni jambo jema na waliunge mkono kwani linatia matumaini.

Anakubaliana na nukuu ya Makala toka kwa mwana mapinduzi wa China, Mao Tsetung ya kwamba ukifanya jambo lolote na ukapingwa na mpinzani wako ujue umepatia endelea nalo na ukifanya jambo na ukaungwa mkono au kupongezwa na mpinzani wako jua kwamba umekosea mahali, acha mara moja mpango huo.

Kwa ufafanuzi huu Makamba anawataka wanachama wa ngazi zote wajiandae kukichangia chama chao na wao wanasubiri kwa hamu mapendekezo hayo ya Idara ili wayatafakari na kupeleka katika ngazi za juu kwa kuyapitisha.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI !!!
Imetolewa na:
Ofisi ya Katibu Mkuu
CCM,Lumumba
1/12/2009

No comments: