Tuesday, August 4, 2009

Rais Kikwete Ashauri Watanzania Kununua Matrekta Badala Magari Ya Anasa

RAIS Jakaya Kikwete ametaja anasa za Watanzania kuwa moja ya mambo yanayofanya sekta ya kilimo kushindwa kufikia malengo ya kuwa uti wa mgongo kwa uchumi wa Tanzania.
Akizungumza katika uzinduzi wa maonyesho ya Nanenane katika viwanja vya Nzuguni nje kidogo ya mji wa Dodoma , Rais Kikwete alisema baadhi ya Watanzania wanapenda zaidi kununua magari ya kifahari badala ya matrekta kwa ajili ya kilimo.

Rais Kikwete alitaja sababu zingine zinazofanya kilimo kisifanikiwe kuwa ni pamoja na ukosefu wa wataalamu wa kufanya utafiti katika sekta ya kilimo

“Watafiti wengi wanaamini kuwa mbegu nzuri ya kupandwa ni ile iliyozalishwa katika maeneo husika sio ya kuagiza kutoka nje, sasa sisi tunaagiza nje asilimia 75 ya mbegu bora zote tunazopanda hapa nchini hiyo ni hatari kwetu” alisema Kikwete.

Katika maonyesho hayo ambayo kaulimbiu yake ni ‘Kilimo kwanza’Mapinduzi ya kijana uhakika wa chakula na kipato,rais alisema haiwezekani kukosa chakula kila mwaka kana kwamba Watanzania wamelaaniwa.

Alisema kila mwaka Tanzania imekuwa ikikosa chakula wakati ardhi ya kutosha ipo pamoja na baadhi ya maeneo kuwa na mvua za uhakika kitu ambacho ni ndoto katika maeneo ya nchi nyingine duniani lakini bado wanazalisha chakula cha kutosha.

Hata hivyo aliponda kwa Watanzania kuendelea kutumia jembe la mkono na akasema kuwa hicho ni kikwazo kingine cha kuwafanya waendelee kubaki katika hali ya umasikini mkubwa ambao utaendelea kuisumbua nchi.

Pamoja na kusema kuwa kilimo cha jembe la mkono kimepitwa na wakati, aliwaacha hoi wakulima pale aliposema kuwa hata kilimo cha jembe la kukokotwa na ng’ombe ni cha zaidi ya miaka 2000 iliyopita.

“Sisi tunahimiza kilimo cha jembe la kukokotwa na wanyama huku tukisahahu kuwa kilimo hicho kilikuwepo tangu hata kabla ya Yesu Kristo kuzaliwa ambayo ni zaidi ya miaka 2000 iliyopita, lakini sisi ndio kwanza tunaanza”

Katika hatua nyingine rais Kikwete amesema Benki ya Wakulima nchini itaanzishwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya China na tajiri maarufu wa Kimarekani Bill Gates.
Rais Kikwete alisema, mkakati huo umekuja kutoka na ukosefu wa vyombo vya fedha vya uhakika vya kutoa mitaji kwa wakulima hapa nchini.

Kikwete alisema serikali imeamua kuchukua hatua hiyo kwa kuwa ukosefu wa mitaji kwa wakulima umekuwa ni kikwazo kikubwa kinarudisha nyuma maendeleo ya kilimo nchini.
Aliongeza kuwa wakulima wengi hawana uwezo wa kununua matrekta kutokana na kuuzwa kwa bei ya juu pamoja na serikali kuondoa kodi kwenye nyenzo hiyo ya kilimo.

“Serikali iligundua uwezo mdogo wa wakulima kununua matreka.Pamoja na kuondoa kodi katika matrekta ili kuwasaidia wakulima lakini bei bado iko juu” alisema Rais Kikwete.
Habari hii imeandaliwa na Habel Chidawali, Patricia Kimelemeta,Dodoma na Hussein Kauli, Dar

Msomaji
Dodoma

1 comment:

Anonymous said...

Mh. rais sisi tunaondesha magari ya anasa lengho letu nikupamba barabara zetu na michuma ya nguvu. CCM nawapongeaza kwa post zenu, pia nitawatumia nyingine nanyie mpendezeshe mtandao wenu. Good job !!!!!