Friday, February 27, 2009

MABADILIKO.

Ulimwengu sasa umebadilika. Mabadiliko au maendeleo yaliyotokea duniani kwa miaka kumi tu iliyopita ni makubwa mno. Dunia sasa imeletwa pamoja na haya maendeleo. Ni rahisi sana sasa kuwasiliana, kusafiri, kufanya biashara hata kuelimisha. Sayansi na teknolojia vimekuwa kiasi kwamba mabadiliko ya mwaka hadi mwaka miaka hii ya elfu mbili ni makubwa kuliko mabadiliko yaliyokuwa yanatokea kati ya miaka mitano wakati wa miaka ya sitini, sabini na themanini. Mabadiliko yatakuwepo na yataendelea kutokea, hivyo swala ni je sisi pia kama wana CCM tunabadilika na haya mabadiliko?

Kitu cha kwanza ninachoona sisi kama wana CCM inabidi mtazamo wetu wa uongozi ubadilike. Kuongoza kwa mtu mmoja bila kuwa na timu kumepitwa na wakati. Inabidi tujifunze kuongoza kwa kushirikiana. Inabidi mshikamano katika uongozi uzidi na kutegemea kichwa cha mtu mmoja kuishe. Kinachotakiwa ni kuwa na malengo ambayo wote tutakubaliana yanahitaji kufikiwa halafu tunaanzisha timu ambazo zitafanya kazi pamoja kwa ushirikiano, heshima na uelewano kuyafikia hayo malengo. Kama kufanikiwa basi tunafanikiwa kama timu na kama kuanguka basi tunaanguka kama timu. Ni miaka ya elfu mbili lakini msemo wa enzi zile wa “kidole kimoja hakivunji chawa” unaweza ukatufundisha mengi sana.

Kitu cha pili ni mawasiliano. Inabidi sisi wana CCM tuwe na uwezo wa kuwasiliana, kupeana habari kadri ya tunavyozipata na kupeana changamoto kadri ya zinavyokuja. Mawasiliana mazuri mara nyingi huwa ndio nguzo ya maelewano mazuri. Na sisi kama jumuia tukielewana vizuri basi tunajiweka katika hali nzuri ya kutimiza malengo yetu kwa pamoja kama timu au kama jumuia. Kuwa na mawasiliano mazuri hakumaanishi kwamba hakutakuwa na kupingana, mawasiliano mazuri ni kwamba hoja zote na mikakati ambayo inabidi iwekwe inajadiliwa kwa kina na kuleta hoja mbadala ambazo zitaleta maendeleo. Ubishi wa kuelimishana na kupeana changamoto lazima uwepo ili kuleta maendeleo.

Cha tatu ni kwamba inabidi sasa tujifunze kusikiliza. Nchi yetu ina watu wa aina tofauti. Kuna makabila tofauti mengi, kuna dini tofauti, na kidemokrasia kuna Vyama vya Kisiasa tofauti. Miaka hii ya mabadiliko ya haraka haraka, inabidi tujifunze kusikiliza wenzetu. Tofauti za aina yoyote ile iwe ni dini ama siasa isiwe kikwazo cha kusikilizana na kupeana ushauri wa maana. Sisi kama wana CCM tuna jukumu la kuwasikiliza wenzetu wa vyama vingine kwani mwisho wa siku sisi wote ni Watanzania na tunaitakia Tanzania mema.kusikilizana ni mwanzo wa kuelimishana. Bila kusikiliza hoja za jirani yako sidhani kama mtu anaweza kuendelea. Kusikiliza wengine kunapanua mawazo na kunaleta hoja mpya. Pia inabidi tuwasikilize wenzetu wa nchi nyingine ili tuibe mawazo ya kimaendeleo. Tunaweza kujifunza mengi sana kama tukisikiliza wenzetu wa ulimwegu huu, tuachane na zile za “sikio la kufa halisikii dawa”.

Kwa kumalizia tu, sisi kama wana CCM inabidi tuwe na mtazamo wa kifikra unaoendana na mabadiliko ya kidunia. Na kama umeshabadilika basi mwambie na jirani yako abadilike na uyaweke hayo mabadiliko katika matumizi ya kuleta maendeleo. Tusijifungie tu na siasa zetu au mawazo yetu bila kuangalia dunia inaelekea wapi. Sisi sasa ni raia wa dunia na chochote tutakachoamua kukifanya basi kitasababisha badiliko au mabadiliko sio Tanzania tu bali ulimwenguni kote. Inabidi tuwaze na tutende katika ngazi sio tu ya kitaifa bali ya kidunia, tukumbuke tu “mgaagaa na upwa, hali wali mkavu”.

Freddie Mwisomba.
United States of America

2 comments:

Anonymous said...

TUNASHUKURU SANA MAWAZO YAKO NDUGU MWANACHAMA

Anonymous said...

wewe una malengho gani ndumgu mwanachama?