Addis Ababa, Ethiopia.
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumanne, Februari 3, 2009, alizima jaribio la kubadilisha msimamo wa Umoja wa Afrika kuhusu mapinduzi ya kijeshi katika Afrika, akisisitiza kuwa kamwe hakuna mapinduzi yoyote ya kijeshi mazuri duniani.
Katika mchango wake uliokatishwa zaidi ya mara nne kwa makofi na mamia ya wajumbe waliofurika katika Ukumbi wa UNCC-ECA mjini Addis Ababa, Ethiopia, kuhudhuria Mkutano wa 12 wa Kawaida wa Umoja wa Afrika (AU), Rais aliwaomba viongozi wenzake wa nchi za Afrika kuwa wakweli katika kujadili masuala muhimu ya maendeleo na ustawi wa Afrika.
Rais Kikwete aliungwa mkono katika hoja yake na baadhi ya viongozi waandamizi wa Afrika akiwamo Rais Idriss Deby wa Chad, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, na Waziri Mkuu wa Ethopia, Zenawi Meles na hivyo kukatisha mjadala huo.
Rais Kikwete aliingilia kati kuzima jaribio hilo baada ya Mwenyekiti mpya wa AU, Kanali Muammar Gaddafi wa Libya, akiungwa mkono na Rais wa Senegal, Abdoulaye Wade kuwasilisha pendekezo kwenye mkutano huo wa kuzirejeshea tena uanachama nchi za Mauritania na Guinea, ambazo zimesimamishwa kwa sababu ya mapinduzi ya kijeshi.
Katika mchango wake, Rais Wade alisema kuwa mapinduzi hasa ya Guinea ni tofauti na mapinduzi mengine ya kijeshi, na kuwa utawala wa kijeshi wa nchi hiyo unaungwa mkono na wananchi.
Rais Wade alitoa uzoefu wake kuhusu utawala huo wa Guinea baada ya kuwa ametembelea nchi hiyo na kudai kuwa aliona jinsi wananchi wa nchi hiyo walivyozitokeza kwa wingi mitaani kumpokea na kuonyesha kuunga mkono utawala huo mpya.
Majeshi katika nchi hizo mbili yalitwaa madaraka katika Guinea na Mauritania mwaka uliopita wakati wa uenyekiti wa Rais Kikwete, ambaye mara moja aliamuru nchi hizo mbili kusimamisha uanachama wa AU kwa mujibu wa maamuzi ya viongozi wa nchi wanachama wa AU.
“Nawaombeni wenzangu tuwe wakweli katika kujadili mambo haya. Ni rahisi sana kwa jeshi kuwapanga watu mitaani na wakashangilia. Na hilo haliwezi kuwa msingi wa kubadilisha uamuzi wa msingi kabisa wa Umoja huu,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Unaweza kufanya lolote ukiwa na bunduki, na niamini mimi kwa sababu nilipata kuwa jeshini. Chini ya utawala wa kijeshi, unaweza hata kuitisha kura ya maoni na kupata asilimia 99,9. Ndugu zangu hebu tuheshimu misingi mikuu ya Umoja wetu kama tulivyokubaliana.
”“Hakuna mapinduzi mazuri ya kijeshi, na lazima tukomeshe utamaduni wa mapinduzi ya kijeshi. Tusirudi nyuma katika miaka ile ya 1960 na 1970. Mtu anayetaka kuwa rais anatakiwa aingie katika siasa na kuomba ridhaa ya wananchi,” alisema, akisisitiza:
“Kama unataka kuwa Rais, unajiuzulu kutoka jeshini.. kama mimi nilivyofanya tena nikiwa na umri mdogo na sasa nimekuwa Rais. Isitoshe, hawa ni watu wanaosema kuwa watakuwa madaraka kwa muda mfupi…lakini angalia yule Lassana Conte wa Guinea aliahidi miaka miwili, akaishia akishikilia madaraka kwa miaka 24.
”Rais Kikwete, kwa hisia na ufasaha mkubwa alielezea historia ya mapinduzi katika Afrika, akitoa mifano ya karibuni zaidi ya mapinduzi katika nchi za Ivory Coast, Guinea, Madagascar na Mauritania. Mwishoni mwa mjadala hata Rais Gaddafi alibadilisha msimamo na kuunga mkono msimamo wa Rais Kikwete na wenzake.
Rais Kikwete aliungwa mkono mara moja na Rais Deby wa Chad ambaye aliwaambia viongozi wenzake: “Kama alivyosema Rais Kikwete, hakuna mapinduzi ya kijeshi mazuri. Tunapoteza muda tu kujadili jambo hilo ambalo tulikwishakulichukua uamuzi….tuache kuzungumzia suala hili, tunapoteza muda tu…
”Naye Rais Museveni alisema kuwa kazi ya jeshi ni kulinda amani ya nchi. “Sasa hawa badala ya kulinda amani ambao ndio wajibu wao wanajaribu kutawala nchi. Hakuna mapinduzi ya kijeshi mazuri na hayajawahi kutokea katika historia. Mapinduzi ya kijeshi ni jam bo lisilokuwa na maana. Ni jambo lisilokuwa na thamani.
”Alisisitiza: “Tokea mwaka 1963, tumekuwa na watu hawa wa kustajabisha…akina Idi Amin. Tutauua Umoja huu kwa mawazo na mijadala ya ovyo na ajabu kama hii. Tuyakatae mapinduzi katika Afrika…na kwenye hili tuko tayari kutofautiana. Hatuwezi kamwe kuzikubali Guinea na Mauritania kurudisha wanachama mpaka zitimize masharti.
”Museveni alisema kuwa yeye ana uzoefu wa kutosha wa kuendesha Serikali zote mbili, ya kijeshi na iliyoingia madarakani kwa kuchaguliwa na wananchi.
“Niamini mimi. Nimekuwa hata mpiganaji wa misituni (rebel). Lakini mchakato wa uchaguzi ni mzuri, unawalazimisha viongozi kufanya kazi. Lakini watu kama Gaddafi wanaukejeli…Ni muhimu kuwapo uchaguzi. Mimi nimeongoza serikali zote mbili, ya kijeshi na isiyokuwa ya kijeshi, najua ninachokisema,” alisisitiza Rais Museveni.
Naye Waziri Mkuu Meles alisema: “Pengine masuala haya ni muhimu lakini siyo ya lazima. Sisi ni viongozi tuache kushinda tunazunguka tu kuhusu hoja zisizokuwa na msingi na kuhusu suala ambalo tayari limeamuliwa. Tuwe na ajenda, vinginevyo tutakuwa sawa na wasusi wa nywele wa jadi katika Ethiopia, ambao kwa sababu wana muda tokea asubuhi hadi jioni, na kwa sababu hawana ajenda, huzungumzia jambo lolote linaloingia kichwani.
”“Hii ni mikutano ya kuzungumzia mambo muhimu na ya maana. Siyo nafasi ya kuja na kupiga picha kwa baadhi ya viongozi,” alisema Meles.
Msomaji,
Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
The world has changed, and we must change with it,” he told an exuberant crowd of hundreds gathered in UNCC-ECA Addis Ababa, Ethiopia. “Starting today, we must pick ourselves up, dust ourselves off, and begin again the work of remaking africa said Kikwete.”
By:
Omari
U S A
Post a Comment