Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wakurugenzi watendaji wa simu za mikononi za Zantel, Tigo na Zain leo jijini Dar es salaam. Kutoka kushoto ni bwana Nabil Tofilis wa kampuni ya Zantel, Pablo Guardia Vasquez kapuni ya Tigo, Khaled Muhtadi kampuni ya Zain, na Rais Kikwete mwenyewe wakwanza kutoka mkono wa kulia.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ya Teknolojia ya Kompyuta – National Fibre Optic – unaojengwa nchini utakuwa na shabaha kuu ya kusukuma mbele maendeleo ya taifa.
Aidha, Rais Kikwete ameelekeza Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kukaa chini na makampuni binafsi ya simu nchini na kuangalia jinsi pande hizo zinavyoweza kushirikiana katika ujenzi wa mkongo huo utakaokuwa na urefu wa kilomita 7,000 ukisambaza mtandao wake katika nchi nzima.
Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo leo, Jumanne, Juni 23, 2009 wakati alipokutana na kuzungumza na viongozi wa makampuni ya simu ya Tigo, Zantel na Zain, Ikulu, mjini Dar Es Salaam.
Rais Kikwete amesema Serikali yake inataka kuyashirikisha makampuni hayo katika ujenzi wa mkongo huo badala ya kila kampuni kufikiria kujenga njia yake yenyewe kwa sababu mkongo huo ni kwa manufaa ya pande zote.
Ujumbe huo ulionana na Rais Kikwete kumweleza nia ya makampuni hayo kutaka kushirikiana na Serikali katika ujenzi huo baada ya makampuni hayo kusita kwa muda mrefu kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa mkongo huo.
Mkongo huo unalenga unalenga kuiwezesha teknolojia ya mawasiliano ya kompyuta kutumika kikamilifu na kwa ufanisi zaidi kwa maendeleo ya taifa.
"Yalikuwa maelekezo yangu na nia yangu tokea mwanzo kushirikisha wadau wote katika ujenzi wa mkongo huo kwa nia ya kupunguza mzigo kwa kila upande kwa sababu mkongo huo utatumiwa na sisi sote," amesema Rais na kuongeza:
"Hayo ndiyo yalikuwa maelekezo yangu kwa Wizara husika, lakini naona awali nyie mlisita kushirikiana na Serikali katika hili," amesisitiza Rais na kuongeza:
"Lakini sasa maadamu mko tayari basi kaeni chini ya wizara husika na kuangalia jinsi ya kukamilisha ujenzi wa mkongo huo."
Mkongo huo unatarajiwa kugharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 170. Serikali imeamua kuzikopa fedha hizo kutoka China ambayo imekubali kutoa mkopo huo.
Rais amewasisitizia viongozi hao wa simu za mkononi kuwa ni muhimu kwa Serikali kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa mkongo huo kwa sababu Serikali inataka mkongo huo utumike kwa ajili ya maendeleo ya taifa na siyo kwa ajili ya faida tu.
"
Tunataka mkongo huu utumike katika kuboresha huduma za elimu, huduma za afya, shughuli za utalii katika kila ncha ya nchi yetu, katika mikoa yote, iwe mijini ama vijijini.
Kwetu sisi ni wajibu wa kitaifa kwa sababu kwa Serikali nia yake kubwa ya kujenga mkongo huu ni kuhakikisha unatumika kwa maendeleo ya nchi." amesema JK.
Msomaji
Dar es salaam
No comments:
Post a Comment