Dk Batilda Buriani akizungumza katika moja ya mikutano mbalimbali aliyowahi kuhutubia kuhusa suala la mazingira.
Serikali imekuwa ikilipa umuhimu mkubwa suala la elimu kwa umma katika kufanikisha programu ya kuhifadhi na kutunza mazingira kwa kutekeleza programu nyingi za elimu ya mazingira kuanzia ngazi ya taifa hadi ngazi ya vijiji.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira Dkt. Batilda Burian wakati akifungua kituo cha elimu na mafunzo ya Mazingira kilichojengwa na kampuni ya Glumeti Fundi kilichopo katika hifadhi ya Serengeti Mkoani Mara.
“Lengo la kutoa programu hizo ni kuielimisha jamii juu ya kuyaelewa mazingira wanayoishi, uhusiano wa shughuli zake za kila siku na ustawi wa mazingira hayo pamoja na kujadili uwiano wake”, alisema Dk. Batilda Burian.
“Grumeti Fund wamefikiria maendeleo ya vizazi vyetu vijavyo hivyo wameamua kuielisha jamii katika kujenga kituo hiki ili rasilimali ya ajabu na ya kipekee iliyopo katika Mbuga ya Serengeti pekee hapa Duniani isiweze kupotea” aliongeza Dk Batilda Buriani.
Akimkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Mstaafu Enos Mfuru alisema kuwa kampuni ya Glumeti Fundi imekuwa ikiwasaidia wananchi wa mkoa huo kwa kuwapatia huduma mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kujenga barabara, kuchimba visima na kutoa elimu kwa jamii
Akieleza nia ya kujengwa kwa kituo hicho Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa maendekeo ya jamii wa Grumeti Grian Harris alisema kuwa kituo cha mazingira ni uwekezaji katika rasilimaliwatu, yaani elimu ya vijana ambapo vijana kumi na wawili pamoja na walimu wao wawili watapata mafunzo kwa muda wa siku tano.
“Baada ya mafunzo ya nadharia na vitendo watakuwa wahamasishaji wa klabu za mali hai kwenye shule yao. Walimu waliioongozana nao watakuwa wasimamizi wao. Wanafunzi wataingia kila wiki na nyakati za likizo, tutaandaa utaratibu wa kuwafunza viongozi wa maeneo ya jirani na hifadhi ya akiba ya Grumeti”, alisema Harris.
Alisema,“Ili kuweza kuyaelewa, kuyakubali na kuishi maisha yanayodumisha mazingira endelevu na yenye tija elimu ni silaha muhimu sana. Kituo cha mazingira kitatoa mchango wake katika kufanikisha ndoto hii”,.Mkurugenzi huyo alimalizia kwa kusema kuwa , wanafunzi wengi kutoka wilaya ya Serengeti na Bunda wamenufaika na wanaendelea kunufaika kielimu kutokana na ufadhili wa Mfuko wa maendekeo ya jamii wa Grumeti.
Tunaahidi kuendelea kufanya hivyo kama sehemu ya wajibu wetu kwa jamii lakini pia kama njia ya endelevu ya kudumisha uhifadhi endelevu.Vijana watakaohudhuria mafunzo kwenye kituo hicho watateuliwa kulingana na ufanisi wao katika masomo yote lakini zaidi elimu viumbe, jiografia na kemia.
Kituo kitawapa changamoto, wakifanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho wachache watafadhiliwa kusomea utalii ama mazingira katika ngazi za vyuo.Gharama ya ujenzi wa kituo hicho ni Shilingi milioni mia nne kumi na mbili na laki tatu za kitanzania. Ikiwa ni gharama ya ujenzi na vifaa vyote katika kuwezesha kituo kiweze kuanza kufanya kazi.
Msomaji
Dar es salaam
No comments:
Post a Comment