Thursday, March 11, 2010

Luhanjo Maafisa Mipango andaeni sera zinatoa majibu ya matatizo ya wananchi

Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo.
Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo ametoa wito kwa wachumi na maafisa mipango kuandaa sera zitakazosaidia kuondoa matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi wa Tanzania katika kujiletea maendeleo yao wenyewe na Taifa kwa ujumla. Alisema kuwa ni wajibu watendaji hao kuandaa sera nzuri zitakazoweza kutoa majibu juu ya matatizo mbalimbali yaliyopo katika jamii ya Tanzania. Luhanjo alisema hayo jana mjini Morogoro wakati anafungua mkutano wa siku tatu wa Maafisa Mipango na wachumi. Alisema kuwa mipango mizuri ni ile inayojaribu kuondoa changamoto zinazokabili jamii kama vile miundo mbinu mibovu, msongamano wa magari mijini, ongezeko la idadi ya watu lisilolingana na rasilimali zilizopo , magonjwa kama vile malaria, UKIMWI na utegemezi wa bajeti kutoka kwa wafadhili. Luhanjo aliongeza ni vema watendaji wakaanda mipango inayotekeleza kwa kuchagua michache ya kipaumbele kulingana na rasilimali zilizopo ili kufanya mipango hiyo kuwa halisi na inayoleta maenendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla. Pamoja na kutoa vipaumbele katika mambo machache , Katibu Mkuu Kiongozi pia aliwaagiza Maafisa hao kuzingatia maelekezo yaliyomo katika Dira ya Taifa 2025 na MKUKUTA ili kuwa na mipango mizuri na michache inayotekelezeka. Alisema wakati umefika kwa Maafisa mipango kuandaa mipango mizuri itakayokuwa ukumbusho wa kazi zao na mchango wao kwa Taifa na raia wake. Mkutano huo ni wa nne kufanyika ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu yake ni jukumu la Maafisa Mipango na maendeleo ya uchumi
Msomaji
Morogoro

No comments: