Wafanyakazi mbalimbali wakiingia katika Uwaja wa Uhuru kwa maandamano leo wakati wa kusherehekea siku ya wafanyakazi Mei Mosi ambayo huadhimisha na wafanyakazi Duniani kote katika kutambua mchangowa wako kwa mataifa husika na nchi zao.
HOTUBA YA RAIS KIKWETE SIKU YA MEI MOSI MUSOMA LEO
Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein akihutubia wananchi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani yaliyofanyika leo Mkoani mara katika uwanja wa Karume Musoma.
HOTUBA
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema serikali itaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kasi ambayo haikuwahi kutokea katika miaka ya nyuma kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu..
Rais Kikwete ameyasema hayo leo mjini Musoma katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein kwenye kilele cha sherehe za Mei mosi zilifanyika kitaifa mkoani Mara.
Rais alisema Tume ya Rais ya kuboresha maslahi ya umma chini ya uongozi wa Ntukamazina imesaidia sana kutengeneza ramani ya (road map) kuelekea kwenye kulipa mishahara inayojitosheleza mahitaji ya maisha.
Alisema utekelezaji wa mengi ya masuala hayo ni ya muda mrefu ambayo yanategemea kuboreka kwa hali ya uchumi wa nchi na kukamilika kwa maboresho yanayoendelea sasa katika utumishi wa umma.
Rais Kikwete alibainisha kuwa katika kipindi ambacho Serikali ya Awamu ya Nne imekuwa madarakani, kuanzia mwaka 2005/2006 hadi 2008/2009, wastani wa mshahara umeongezeka kutoka shilingi 152,849 hadi shilingi 296,631 kwa mwezi, ikiwa ni ongezeko la asilimia 94 kiasi kwamba kima cha chini kimeongezeka kutoka shilingi 65,000 hadi shilingi 100,000 kwa mwezi.
“Sisi katika serikali, tafsiri yetu ya maslahi ya wafanyakazi inajumuisha yote haya. Tunayazingatia nyote haya katika kutekeleza azma yetu ya dhati ya kuboresha maslahi ya umma”, alieleza
Alisema mwanzoni serikali ilikadiria uchumi wa nchi ungekuwa kwa asilimia 8 mwaka huu lakini kutokana na msukosuko wa uchumi duniani kasi ya ukuaji wa uchumi itapungua na unatarajiwa kukua kwa kati ya asilimi 5-6 hali ambayo itaathiri uwezo wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi kama ilivyozoeleka.
Rais alisisitiza pia kuwa serikali itaendelea kuyatambua madai ya mara kwa mara ya kuongezwa mishahara ya wafanyakazi kwa kuwa ni madai halali kabisa.
Hata hivyo alisema ni muhimu kukumbuka kwamba maslahi ya wafanyakazi hayaishii kwenye mishahara peke yake kutokana na ukweli kwamba yapo masuala ya uhakika wa kazi, usalama kazini, maslahi ya kustaafu, ushirikishwaji wa wafanyakazi na mambo yahusuyo afya, bima na maendeleo ya elimu ya wafanyakazi.
Kuhusu maslahi ya wafanyakazi kwenye sekta binafsi Rais alisema serikali imefanya jitihada kwa kushirikiana na wadau, ikiwemo waajiri na vyama vya wafanyakazi kuhakikisha mishahara hiyo inaongezwa kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi wa sekta mbalimbali.
“Kwa mfano, katika sekta ya madini, mishahara iliongezwa kutoka shilingi 48,000 kwa mwezi mwaka 2005 hadi 350,000 kwa mwezi mwaka huu”, alieleza.
Aidha Rais Kikwete alisema serikali ina mpango wa kuanzisha mamlaka itakayokuwa na wajibu wa kuratibu, kusimamia na kutoa miongozo kwa sekta ya hifadhi ya jamii ambayo itasaidia kupunguza malalamiko kuhusu utendaji wa Mifuko iliyopo sasa.
Aliwataka wafanyakazi kuwa mstari wa mbele katika kukataa kutoa na kupokea rushwa katika maeneo yao ya kazi na wasisite kuwaripoti katika vyombo vya kisheria wale wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Katika sherehe hizo Makamu wa Rais alikagua mabanda ya maonyesho, alitoa nishani kwa waasisi wa vyama vya wafanyakazi Mzee Rashid Kawawa, Joseph Rwegasira na Alfred Tandau, alikabidhi zawadi kwa wazee wastaafu watano kutoka mkoa wa Mara pamoja na wafanyakazi bora wa kitaifa na washindi wa michezo ya Mei Mosi
No comments:
Post a Comment