Monday, April 12, 2010

Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete, katibu Mkuu wa CCM Yusuf Makamba(katikati) na makamu mwenyekiti CCM Bara Pius Msekwa(kulia) wakituma ujumbe mfupi sms kupitia simu zao ili kuchangia CCM wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuchangia CCM kupitia simu za mikononi ulifanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar
Habari zaidi kutoka Magazetini:
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kutumia Sh bilioni 1.5 kukodishia helikopta na ndege katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Fedha hizo ni kati ya Sh bilioni 40 wanazotarajia kuchangisha kwa ajili ya uchaguzi huo kupitia wanachama wake kwa njia ya ujumbe mfupi, akaunti ya benki na harambee.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Rais Jakaya Kikwete wakati akizindua rasmi kampeni za uchangiaji wa chama katika hafla iliyofanyika juzi usiku na kuwashirikisha viongozi wa juu wa chama hicho.

Kikwete alisema wameamua kukodisha helikopta na ndege ili kuepuka adha walizokuwa wakikumbana nazo katika kampeni za uchaguzi uliopita.

Mbali na ndege, pia Kikwete alisema kuwa katika malengo yao ya kuchangisha Sh bilioni 40 tayari wamepata Sh bilioni 4.8 ambazo zimechangishwa kupitia akaunti namba 01j1005069306 katika Benki ya CRDB.

CCM inatarajia kukusanya Sh bilioni 4.4 kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS) ambapo muda mfupi baada ya kuzindua kampeni hiyo, SMS 20,000 zilitumwa katika kipindi kifupi kisichozidi saa nne.

Katika njia hiyo wachangiaji wanatakiwa kutuma neno CCM kwenda namba 15399 ambapo watakuwa wamechangia Sh 1000 na wakituma kwenda namba 15388 watachangia Sh 500 na kwenda namba 15377 watachangia Sh 300.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Uchangiaji na Katibu wa Uchumi na Fedha wa chama hicho, Amos Makala alisema kuwa CCM ina wagombea 2,932 katika ngazi zote nchi nzima.

Alisema kuwa kwa kuwa ndio chama pekee kinachosimamisha wagombea katika ngazi zote za uchaguzi, kinatarajiwa kutumia Sh bilioni 3 katika kuendesha shughuli za kuchagua wagombea watakaogombea nafasi mbalimbali.

Alisema kuwa Sh bilioni 5 zinahitajika kwa ajili ya kununulia magari 26 kwa Tanzania bara huku Zanzibar ikihitaji magari 60. Pia watanunua pikipiki elfu sabini pamoja na baiskeli elfu 25 ambapo kwa pamoja itagharimu Sh bilioni 2.5.

Makala alisema kuwa kwa ujumla gharama ilitakiwa kuwa Sh bilioni 50 lakini magari yaliyopo katika ngazi za wilaya yamepunguza gharama mpaka kufikia Sh bilioni 40.

" Najua kwa kuwa CCM ndio chama ambacho kimekuwa kikiongoza nchi kwa muda mrefu, naona kuwa inatakiwa wanachama na wale wanaokitakia mema chama kutumia njia zilizo sahihi kwao kutuchangia fedha kwa ajili ya uchaguzi huu,” alisema Makala.

Alifafanua zaidi kuwa Sh bilioni 10 zinahitajika kwa njia ya harambee ambapo alisema kuwa kampeni ya kupata fedha kwa njia hiyo itazinduliwa.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na mawaziri wakuu wastaafu akiwemo Edward Lowassa, John Malecela na David Msuya.

No comments: