Friday, September 18, 2009

Ngeleja: Matumizi ya nishati mbadala huleta maendeleo endelevu

Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja.
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, amesema matumizi ya nishati mbadala, nishati isiyoharibu mazingira na magari yatumiayo nishati isiyoharibu mazingira ni kichocheo cha maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi duniani kinachohifadhi na kutunza mazingira.

Waziri Ngeleja ameyasema hayo katika Mkutano wa Dunia wa kujadili nishati mbadala na matumizi ya magari yanayotumia nishati isiyoharibu mazingira ‘clean vehicles’ pamoja na nishati isiyoharibu mazingira ‘clean fuels’, unaofanyika mjini Stockholm nchini Sweden kuanzia Septemba 16 hadi 18 mwaka huu.

“Tanzania imekuwa ikipiga hatua katika kuzalisha nishati za umeme zitokanazo na maji, upepo, gesi asilia, jua na umeme unaozalishwa kwa kutumia makaa ya mawe ‘geothermal’ lakini rasilimali kama upepo, umeme wa makaa ya mawe, madini ya uranium na nishati ya mawimbi hazijaanza kushughulikiwa”, alisema.

Kwa mujibu wa Waziri Ngeleja, asilimia 90 ya nishati itumiwayo Tanzania inatokana na mimea mfano kuni na mkaa wakati asilimia nane hutokana na nishati ya kuagiza nje inayotokana na petroli huku asilimia 1.5 hutokana na nishati ya umeme inayozalishwa kwa kutumia maji, gesi asilia na makaa ya mawe.

Alisema kuwa asilimia 0.5 ya nishati inayotumiwa hapa Tanzania hutokana na upepo, umeme wa jua na rasilimali nyingine zitoazo nishati.

Mbali na hayo, Waziri Ngeleja ameueleza mkutano huo kuwa Tanzania ina fursa ya kuwa na maendeleo endelevu yatokanayo na matumizi ya nishati mbadala kwa sababu ina hali ya hewa nzuri inayoruhusu kustawi kwa mimea inayotoa nishati, ipo katika ukanda unaoruhusu biashara ya nishati hiyo kwa sababu inatumia Bahari ya Hindi kwa pamoja na nchi nane jirani.

Pamoja na mafanikio yanayopatikana kutokana na matumizi ya nishati mbadala, Waziri Ngeleja alisema kuna changamoto ambazo zinaikabili Tanzania ikiwa ni nchi changa katika matumizi ya nishati hii ya kisasa.Aliitaja changamoto ya kwanza ni kuwa ni mdororo wa kiuchumi ulioikumba Dunia na kuathiri sekta ya uwekezaji.Mbali na hilo, anasema utunzaji wa mazingira na uendelezaji wa nishati mbadala unahitaji mipango na mikakati ya uhakika ambayo Tanzania inaichukua kwa umakini mkubwa

Msomaji
Dar es salaam

No comments: