Thursday, September 10, 2009

Taarifa Rasmi: Kuhusu Kikao Cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM

Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imefanya Mkutano wa kawaida tarehe 16-17 Agosti, 2009 chini ya Uenyekiti wa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

Katika mkutano huu Halmashauri Kuu imejadili masuala mbali mbali kuhusu hali ya kisiasa nchini, maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura, pia imefanya uteuzi wa wagombea katika nafasi mbalimbali.

Baada ya kujadili masuala hayo, Halmashauri Kuu ya Taifa imefanya maamuzi yafuatayo:-

1. MAANDALIZI YA UCHAGUZI

(a) Serikali za MitaaHalmashauri Kuu ya Taifa imepitisha ratiba ya CCM kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa; kwa mujibu wa ratiba hiyo muda wa kuchukua na kurudisha fomu kwa wagombea wa CCM kwa uongozi wa Vitongoji, Serikali za Vijiji na Mitaa ni toka tarehe 10/8/2009 hadi 20/8/2009.

Halmashauri Kuu ya Taifa imetoa wito kwa wana CCM na wapenzi wa CCM katika ngazi ya Vitongoji, Vijiji na Mitaa wajiandae kushiriki kwa ukamilifu katika mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu kwa kuzingatia ratiba ya CCM na pia ratiba ya wasimamizi wa Uchaguzi huu (TAMISEMI).

Aidha, Halmashauri Kuu ya Taifa imewahimiza wana CCM na wapenzi wa CCM wajitokeze kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura kuanzia tarehe 4/9/2009 hadi 25/9/2009 na kwamba muda ukiwadia wajitokeze kuwapigia kura wagombea wa Chama Cha Mapinduzi hapo tarehe 25/10/2009.

(b) Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura - Pemba
Halmashauri Kuu ya Taifa baada ya kupokea taarifa kuhusu zoezi la uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura Kisiwani Pemba, imetoa wito kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ihakikishe zoezi hilo linasimamiwa kwa makini, na liendeshwe kwa haki na kwa utulivu; na kwamba Serikali ya Mapinduzi ihakikishe kwamba kila mwenye haki na sifa ya kujiandikisha anapata haki hiyo, na wale wasio na sifa wasiruhusiwe kujiandikisha.Kimsingi zoezi hili sharti liendeshwe kwa kuzingatia sheria ya Uchaguzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na sio vinginevyo.


2. KUONGEZA IDADI YA WANAWAKE KATIKA VYOMBO VYA UWAKILISHI

Halmashauri Kuu ya Taifa imetafakari upya mapendekezo yake ya awali kuhusu utaratibu wa kuongeza idadi ya wanawake katika Bunge la Muungano na katika Baraza la Wawakilishi. Mapendekezo mapya ni kama ifuatavyo:-

(a) Kwamba kwa kuwa idadi ya Wabunge wote kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 66(1)(b) ni 249, viti asilimia arobaini (40%) itengwe kwa ajili ya wanawake, yaani viti 100.

(b) Kwamba ukomo wa viti Bungeni ubaki 360, hivyo pendekezo hili litaongeza idadi ya viti kutoka 323 vya sasa hadi 349, na vitabaki viti 11 kufikia ukomo wa viti (360) Bungeni. Hali hii inawezesha Tume ya Uchaguzi kuongeza idadi ya majimbo mapya 11.

(c) Utaratibu wa asilimia 40 utakapotumika utawezesha kupatikana kwa Wabunge Wanawake 100 kwa viti maalum pekee, idadi ambayo ikijumulishwa na wa kuchaguliwa ambao kwa sasa ni 18, watano wa kuteuliwa na wawili kutoka Baraza la Wawakilishi, tutapata Wabunge wanawake 125. Kiwango hiki ni sawa na asilimia 50 ya Wabunge wote waliotajwa kwenye Ibara ya 66(1) (b) ya Katiba.

(d) Ili kufikia lengo la kupata wabunge wanawake 50%, wanawake hawana budi kushindana kwa bidii katika majimbo. Kwa hali hii Halmashauri Kuu ya Taifa imeagiza CCM katika ngazi zote zifanye uhamasishaji wa Wanawake wengi kwenda kugombea katika majimbo ya uchaguzi mwaka 2010 ili kuongeza Wabunge zaidi ya 18 waliopo hivi sasa.

3. UTEUZI WA WAGOMBEA UENYEKITI WA WILAYA

Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, imepitisha wana CCM walioomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa CCM katika Wilaya za Rorya, Tarime na Arumeru.Nafasi za Tarime na Rorya zimetokana na kugawanywa kwa wilaya ya Tarime na kuwa wilaya mbili na ile ya wilaya ya Arumeru imetokana na kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Wilaya hiyo, Ndugu Lucas Lobulu aliyefariki Mei 6, 2009. Waliopitishwa kugombea nafasi hizo ni:-

Wilaya ya Arumeru
1.Ndugu Jeremiah Saruni Kaaya
2. Ndugu Gabriel Kilale Nnko
3.Ndugu Joseph Ole Loning’o Saivoiye

Wilaya ya Tarime
1.Ndugu George Mkama Chacha
2.Ndugu Bogomba Rashid Chichake
3.Ndugu Peter Keba Wangwe

Wilaya ya Rorya
1.Ndugu Leonard Yodal Ambonya
2.Ndugu Jomoko Mjee Kateti
3.Ndugu Ramadhan A. Nyanganira

Wilaya husika zitafanya uchaguzi kwa ratiba itakayoandaliwa baadaye.

4. CHAGUZI NDOGO BUSANDA, MAGOGONI NA BIHARAMULO

Baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa kujadili tathmini ya chaguzi ndogo katika majimbo ya Busanda, Magogoni na Biharamulo, imewashukuru na kuwapongeza wale wote waliofaikisha ushindi wa CCM katika Uchaguzi mdogo wa Majimbo ya Ubunge ya Busanda (Mwanza) na Biharamulo Magharibi (Kagera) pamoja na Uchaguzi mdogo wa Uwakilishi wa Jimbo la Magogoni, Zanzibar.

Aidha, Halmashari Kuu pia imetoa pongezi za dhati kwa wana-CCM, wapenzi wa CCM na wananchi kwa ujumla kwa ushindi waliokipatia Chama Cha Mapinduzi katika chaguzi hizo ndogo za Ubunge, Uwakilishi na za Udiwani katika Kata 10 za Tanzania Bara.Kutokana na ushindi huo, kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kiliwaomba wana-CCM, wapenzi wa CCM, wakereketwa na wananchi kwa ujumla kuendelea kukipa ushindi Chama Cha Mapinduzi ili kiendelee na majukumu ya kumkomboa Mtanzania na kudumisha amani na utulivu.

5. MAHAKAMA YA KADHI

Halmashauri Kuu ya Taifa imeridhika na hatua zinazochukuliwa na Serikali za kulipatia ufumbuzi suala la Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara. Moja ya hatua hizo ni uundaji wa Kamati ya mazungumzo baina ya viongozi wa dini ya Kiislam na Serikali kuhusu mchakato wa uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi nje ya mfumo wa Serikali.

Aidha, Halmashauri Kuu imesisitiza kwamba iwapo wapo Waislam wanaona haki zao hazikamiliki bila ya kuwa na chombo cha aina hiyo, wasizuiliwe. Waruhusiwe kuanzisha Mahakama ya Kadhi wao wenyewe na Serikali isijihusishe kuiendesha mahakama hiyo kwani kwa kufanya hivyo itakuwa imejiingiza katika shughuli za kidini; na kwamba Mahakama hiyo isihusike na kesi za jinai wala madai, bali ihusike na masuala ya ndoa, talaka na mirathi.

6. WARAKA WA BARAZA LA MAASKOFU (RC)

Baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa kuzingatia waraka wa Maaskofu, na hasa malumbano na hisia tofauti zilizojitokeza kuhusu waraka huo, imeelekeza kwamba viongozi wakuu wa nchi wafanye mazungumzo na viongozi wa dini zote ili kutafuta njia tulivu ya kusafisha hali ya hewa na kujenga umoja na utengamano katika jamii yetu.

7. MALUMBANO YA VIONGOZI

Kuhusu tabia iliyozuka hivi karibuni ya baadhi ya Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Viongozi wa Chama kutoa matamshi hadharani yenye mwelekeo wa kuchafuana majina, na yanayoashiria kuvunjika kwa umoja na mshikamano ndani ya CCM na Serikali zetu, na pia yenye mwelekeo ya kudhoofisha muungano wetu, Halmashauri Kuu ya Taifa pamoja na kukemea vikali tabia hii, imetoa maagizo yafuatayo:-

(a) Kwamba kuanzia sasa viongozi wote wa CCM warejee katika nidhamu ya Chama ya kuzungumzia masuala ya Chama katika vikao rasmi vya Chama na sio vinginevyo.

(b) Kamati za Wabunge wa CCM, na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM zitumike kujadili masuala yahusuyo CCM ndani ya vyombo hivyo.

(c) Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar watumie taratibu zilizopo katika kushughulikia kero za Muungano badala ya kufanya kwa suala la mafuta kwa upande wa Zanzibar.

d) Viongozi watakao vunja maadili haya watakuwa wamejibainisha kwamba hawana nia njema na CCM, na watahesabiwa ni wasaliti wa CCM hivyo Chama hakitasita kuwapa adhabu kali, ikiwa ni pamoja ya kuvuliwa uongozi na hata kufukuzwa katika Chama.

(e) Halmashauri Kuu ya Taifa imetoa wito kwamba mapambano dhidi ya rushwa na maovu mengine ni jukumu la wana CCM wote na raia wema wote kwa mujibu wa Katiba ya CCM Ahadi 4 ya Wana CCM. Halmashauri Kuu ya Taifa imeonya kuhusu dhana inayojengeka kwamba vita dhidi ya rushwa na ufisadi inahusu kikundi kidogo tu cha wana CCM, usahihi ni kwamba vita hii ni ya wana CCM wote kwa mujibu wa Katiba ya CCM vita hivi lazima iendelee kuhusisha wana CCM wote na wananchi wote wenye mapenzi mema na nchi yetu.

(f) Kwa kutambua kuwepo matatizo ya matamshi na vitendo visivyoridhisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi, Halmashauri Kuu ya Taifa imeamua kuunda Kamati Ndogo ya kutafuta undani wa matatizo hayo na kupendekeza kwa Kamati Kuu njia za kuyatatua. Aidha, Kamati hiyo pia itaangalia utendaji kazi wa Kamati za Chama katika Bunge na Baraza la Wawakilishi kwa nia ya kubaini upungufu uliopo ili kupendekeza kwa Kamati Kuu kuhusu njia za kurekebisha. Pia, Kamati itaangalia masuala ya uendeshaji wa shughuli za Bunge na Baraza la Wawakilishi na kushauri namna ya kuimarisha, pale panapostahili.

Kamati hiyo itaongozwa na Mzee Alli Hassan Mwinyi Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Wajumbe wengine ni Mzee Pius Msekwa Makamu Mwenyekiti CCM (Bara) na Ndugu Abdulhaman Kinana.

8. KUHESHIMU VIONGOZI WASTAAFU

Halmashauri Kuu ya Taifa imewakumbusha wana CCM, Viongozi na Watanzania kwa jumla kuhusu umuhimu wa kudumisha utamaduni wa kuwaheshimu na kuwaenzi viongozi wastaafu, hususan Marais wastaafu.

Aidha, Halmashauri Kuu ya Taifa imesikitishwa sana na hali iliyojitokeza Bungeni ya kutoa maneno ya kejeli dhidi ya Mzee Benjamin W. Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu.

Halmashauri Kuu ya Taifa imesisitiza kwamba Mzee Mkapa katika kipindi chake ameliongoza Taifa letu kwa ufanisi mkubwa, aliinua hali ya uchumi, aliendeleza miundombinu, aliendeleza huduma za kijamii hasa elimu, afya, maji na kwa jumla alilijengea heshima kubwa Taifa letu.

Mzee Mkapa anastahili pongezi sio kejeli, anastahili heshima na sio dharau, anastahili kuenziwa na sio matusi.

Kwa kuzingatia hayo, Halmashauri Kuu ya Taifa inatoa wito kwa wana CCM na Watanzania wote wenye nia njema na nchi yetu waache mara moja kumchafua na kumkejeli Mzee Mkapa na badala yake apewe heshima anayostahili na aachwe apumzike kwa amani.

9.UTEUZI WA MAKATIBU WAPYA WA MIKOA

Halmashauri Kuu ya Taifa imewateua wafuatao kuwa Makatibu wa Mikoa:-

(1) Ndugu Sauda Mpembalyoto (Katibu wa Wilaya ya Hai)
(2) Capt. (Mst) Frarten Kiwango (Katibu wa Wilaya ya Kibaha Mjini)

Hawa wanajaza nafasi zilizoachwa wazi na Ndugu Amina Makilai aliyekuwa Katibu wa Mkoa wa Pwani na sasa ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UWT, pia Ndugu Salum Msabah aliyekuwa Katibu wa Mkoa wa Kigoma na sasa amerejeshwa Makao Makuu ya CCM kuongoza Kitengo cha Propaganda.

10. UCHAGUZI WA MJUMBE WA NEC KUPITIA JUMUIYA YA WAZAZI

Nafasi hii iliachwa wazi na marehemu Richard Nyaulawa na ilikuwa inawaniwa na wagombea watatu.Kutokana na kura za wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa aliyechaguliwa ni Ndugu Jasson Rweikiza aliyepata kura 88.

Wengine waliogombea nafasi hii ni Ndugu Ramadhani Maneno kura 85 na Ndugu Sifa Swai kura 46.

Imetayarishwa...11:50:20 17.08.2009.
MAKAO MAKUU,
CHAMA CHA MAPINDUZI
DA ES SALAAM

No comments: