Saturday, November 26, 2011

Nape afanya ziara Tawini CCM Marekani


Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa Mh Nape Nnauye alifanya ziara ya kikazi nchi Marekani na kutembelea tawi la CCM Marekani mjini Houston.


Katika siku yake ya kwanza Mh Nape aliongea na viongozi wa Tawi katika mkutano wa ndani wa kikazi. Mh Nape alisisitiza umuhimu wa matawi ya nje kuwa mabalozi wazuri wa chama na nchi kwa ujumla. Alilitaka tawi hili kuongeza nguvu na kuwafikia wananchama wengi zaidi ndani ya Marekani. Alitoa wito wa Tawi hili kuwa chachu ya kuongezeka kwa matawi mengine mengi na kuongeza nguvu ya chama ndani ya Marekani. Mh Nape ambaye aliambatana na Katibu Mkuu Msaidizi wa Idara ya Itikadi na Uenezi Ndg. Sixtus Mapunda alitoa rai ya kulitaka tawi la CCM Marekani ambalo lipo Houston, Texas kujiunda kama tawi CCM Texas ili kutoa nafasi kwa matawi mengine kuundwa katika maeneo au majimbo mengine ambayo yanawiana kijiografia ndani ya nchi hii. Alibainisha kuwa ukubwa wa nchi ya Marekani unahitaji maeneo tofauti kuunda matawi kamili ili kufanikisha na kurahisisha shughuli za kichama.


Awali kabla ya kumkaribisha Mh Nape kuongea na viongozi wa tawi, Kaimu Mwenyekiti wa Tawi la CCM Marekani Mh. Amina Lesso alimshukuru Katibu wa itikadi na Uenezi - Taifa pamoja na ujumbe wake kwa kuweza kufika tawini hapa na kuimarisha nguvu za CCM hapa Marekani. Mh Lesso aliomba ziara kama hizi zisiwe mwisho bali ndiyo ziwe zimefungua mlango kwa viongozi wengine wa kitaifa kufika Houston na kutembelea tawi na shughuli zetu za chama.


Mh Nape kesho yake alitarajiwa kufanya mkutano na wanachana na watanzania waishio Houston na maeneo mengine ya jirani.

No comments: