Monday, February 27, 2012

Mabadiliko ya Katiba ya CCM



CHAMA Cha Mapinduzi kimefanya mabadiliko ya Katiba yake ya mwaka 1977 toleo la 2010 na kanuni zake, baada ya Halmashauri kuu ya chama hicho chini ya Mwenyekiti wake wa taifa Rais Jakaya Kikwete.Mabadiliko ya katiba ya CCMAkielezea mabadiliko hayo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye anasema, kwanza Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imebadili namna ambavyo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inavyopatikana.“Wajumbe hao waliokuwa wakipatikana kutoka kwenye ngazi ya mikoa, sasa wamegawanywa katika makundi sita ambayo ni ngazi ya Taifa itakayokuwa na wajumbe 10 kutoka Tanzania Bara na wajumbe 10 kutoka Tanzania visiwani” anasema na kuongeza, “Kundi la pili litahusisha wajumbe 10 wa kuteuliwa na mwenyekiti wa CCM Taifa. Kundi la tatu linahusisha wajumbe wanaoingia kwa nafasi zao wakati kundi la nne lina wajumbe wanaotoka kwenye vyombo vya uwakilishi kama vile wanaochaguliwa na Bunge nafasi 10 (Bara nafasi nane, Zanzibar nafasi mbili), wanaochaguliwa, Bara tano na Zanzibar nafasi tano)”. Analitaja kundi la tano linalohusisha wajumbe wanaochaguliwa kutoka wilayani nafasi 221. Wajumbe hao waliochaguliwa kupitia wilaya watakuwa ni viongozi wa kazi za muda wote ili kuweka wazi zaidi wajibu wa wajumbe hao wa kuwa karibu na wanachama na kushughulikia shida zao.Kundi la mwisho ni wajumbe toka kwenye jumuiya za chama, kama vile wanaochaguliwa na Umoja wa Wanawake nafasi 15 (Bara nafasi tisa na Zanzibar nafasi sita). “Umoja wa Vijana (UVCCM) nafasi 10 (Bara nafasi sita na Zanzibar nafasi nne). Jumuiya ya Wazazi nafasi tano(Bara nafasi tatu na Zanzibar nafasi mbili)”. Baraza la UshauriKatika mabadiliko hayo Halmashauri kuu ya Taifa imeamua kuwa viongozi wakuu wastaafu ngazi ya taifa waundiwe baraza la ushauri.Nape amesema kuwa, Baraza hilo litakuwa na wajumbe kama vile Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao walikuwa wenyeviti wa CCM Taifa. Anawataja wengine kuwa ni pamoja na Marais wastaafu wa Zanzibar ambao pia walikuwa Makamu wenyeviti wa CCM Taifa na Makamu wa mwenyekiti wa CCM Taifa wastaafu.“Baraza litakuwa na kazi ya kutoa ushauri kwa Chama na serikali zinazoongozwa na CCM, kwa madhumuni hayo hayo katika jambo mahsusi. Wajumbe wa baraza hilo wanaweza pia kualikwa ama wote au mwakilishi wao kuhudhuria vikao vya chama ngazi ya Taifa” anasema Nape.Mabadiliko ya Katiba na mbio za urais ndani ya CCMWakati CCM kikifanya mabadiliko hayo, kumekuwa na hofu ya kuwapo kwa mkakati wa kuwadhibiti baadhi ya makada wa chama hicho waliopani kugombea urais mwaka 2015. Hofu hiyo inaelezwa kuwa ni kutokana na kubadilisha namna ya kuwapata wajumbe wa NEC kutoka ngazi ya mikoa hadi wilaya ikiwa ni mkakati wa kuyadhibiti makundi yanayoweza kutumia nguvu ya fedha kuwanunua wajumbe hao kwa malengo yao binafsiJapo chama hicho hakijaanza rasmi mchakato wa kutafuta mgombea urais, tayari baadhi ya makada wametajwa kupita huko na huko ili ‘kujiuza’. Makada hao wameonekana wakipita makanisani na misikitini, wakishiriki ibada na kufanya harambee na matamasha, hali inayotafsiriwa kuwa ni mikakati ya kujitangaza.Baadhi ya makada wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi Hussein Mwinyi na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri Mkuu wa sasa Mizengo Pinda. Wengine ni pamoja na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Utawala Bora Mathias Chikawe, Waziri wa Ujenzi John Magufuli, Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Lazaro Nyalandu na Waziri wa Maliasili na Utalii Ezekiel Maige. Hata hivyo kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanaotajwa wamekanusha vikali kuhusika na mbio hizo. Kati ya waliojitokeza hadharani na kukanusha mikakati hiyo ni pamoja na Samuel Sitta ambaye amesema kama ni urais utamfuata mwenyewe, siyo yeye kuutafuta. Naye Waziri Mkuu Pinda amesema kuwa urais ni mzigo ambao asingependa kuubeba. Naye Lazaro Nyalandu amekanusha si tu kujihusisha na mbio hizo bali hata kushirikiana na wanaokimbilia. Hata hivyo, hofu hiyo imekanushwa na Katibu wa Itikadi na uenezi Nape Nnauye akisema kuwa hakuna sababu ya kuwa na hofu ya kuzuiwa kugombea urais kwasababu tu kushindwa kuingia kwenye NEC. “Sifa ya msingi kwa mtu kugombea urais kwa mujibu wa Katiba yetu, kwanza ni mtu huyo kuwa mwanachama wetu, awe ni mbunge au asiwe,” anasema Nape na kuongeza; “Nimekuwa nikisema mara kwa mara kwamba, hii ni sehemu tu ya mkakati wa kujivua gamba tuliyokuwa tukiitangaza. Hakuna anayelengwa hapa. Yeyote anayedhani kuwa hawezi kugombea urais bila kuwa mjumbe wa NEC, basi hilo ni tatizo na ninaweza kusema kuwa huyo amefilisika kisiasa” anasema Nape. Mbali na kipengele hicho cha kuwapata wajumbe wa NEC, suala la kuunda Baraza la Ushauri linalowahusisha viongozi wastaafu nalo limewekewa alama ya kuuliza kwamba, je, nao ni mkakati mwingine wa kuwadhibiti wagombea urais?Hata hivyo akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam, hivi karibuni, Nape amesema uundwaji wa Baraza la Ushauri la Wazee umetokana na mawazo ya wazee wenyewe wastaafu wa chama hicho ambao wamebaini ipo haja ya kuwa na chombo hicho kutokana na sababu mbalimbali.“Jambo kubwa ambalo linapotoshwa sana ni la uamuzi wa NEC kuunda Baraza la Ushauri la Wazee. Uamuzi ambao kimsingi ulifikiwa kwenye kikao cha NEC cha mwezi Aprili mwaka 2011 Mjini Dodoma kikao ambacho kiliridhia kufanyika kwa mageuzi ndani ya Chama. Kikao cha February 12, 2012 cha NEC kiliridhia tu mabadiliko ya katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2010 ili kuruhusu kuundwa kwa baraza hilo,” anasema Nape.Ameongeza kuwa, wazo la kuundwa kwa baraza hilo limetokana na ushauri wa baadhi ya wazee wenyewe wastaafu wakizingatia wingi na urefu wa vikao husika, na si mpango au mkakati wa kuwaengua makusudi wastaafu hao kama inavyodaiwa na baadhi ya wapotoshaji.“Ilikuwa ni ushauri wao kwamba baada ya kustaafu badala ya kulazimika kuhudhuria vikao vya kitaifa kila mara basi wapewe muda wa kupumzika na wanapotakiwa kutoa ushauri watumiwe badala ya utaratibu wa sasa wa kulazimika kuhudhuria vikao ambavyo kwakweli ni vingi na wakati mwingine huisha usiku wa manane,” anasema na kuongeza; “Baada ya wazo la wazee wetu kupumzika, huku tukizingatia kuwa busara zao bado ni muhimu sana kwa Chama na Taifa, busara ikatumika badala ya kupumzika kabisa basi tuunde Baraza la Ushauri la Viongozi wa Kitaifa wastaafu. Na hii haina maana kuwa hawaruhusiwi kuhudhuria vikao vya Chama na kuwa hawatatumika kwa kazi za Chama na Taifa kwa ujumla, isipokuwa mabadiliko haya yanaondoa ulazima wa wao kuhudhuria vikao hivyo kama ilivyokuwa mwanzo.” Pamoja na hayo ameongeza kuwa CCM imebaini chama makini chochote kitatafuta utaratibu bora wa kuwaenzi waasisi wake na kuendelea kuvuna busara na hekima zao katika kuendelea kukijenga Chama. Katika hili CCM imeonyesha mfano mzuri unaostahili kuigwa na vyama vingine. Kuundwa kwa baraza hili na kutambuliwa rasmi na katiba ya Chama ni uthibitisho tosha wa namna CCM inavyothamini wastaafu hawa. “Chama Cha Mapinduzi kinathamini sana busara na mchango wa wastaafu hawa katika ujenzi wa Chama na Taifa kwa ujumla hakiwezi kuwaong’oa au kuwatupa kama inavyojaribu kupotoshwa na baadhi ya watu. Tuwatendee haki wazee wetu hawa badala ya kutumia vibaya majina yao na uamuzi wa Chama ambao una baraka zao,” anasema Nape.

No comments: