Sunday, August 22, 2010
CCM yaanza kampeni kwa kishindo
Rekodi iliyowekwa na Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete katika kutimiza ahadi zake, ni kielelezo tosha cha kukichagua chama hicho kuendelea kuiongoza nchi. Hatua hiyo ndiyo inafanya mgombea urais wa chama hicho, Kikwete aamini, kwamba CCM safari hii itashinda kwa kishindo zaidi, katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 31, mwaka huu. Akizindua rasmi kampeni za uchaguzi za CCM katika viwanja vya Jangwani Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema: “Hatuwaangusha … tumetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005 kwa kiwango kikubwa sana, yapo machache ambayo hatujayakamilisha na ambayo tutayachukua ili kuyakamilisha katika Ilani ya 2010”. Alisema CCM ni chama kinachoaminika na Watanzania wengi kutokana na uimara na ubora wa sera, ubora wa muundo na ubora wa wagombea wake, na kuwataka wananchi kuendelea kukiamini kwa kuchagua wagombea wake katika uchaguzi mkuu ujao. “Vipo vyama saba ambavyo vimesimamisha mgombea kwa nafasi ya Rais wa Jamhuri, lakini mgombea wa CCM ni bora zaidi. Tumejaribu kuangalia sera za vyama vyote 13 vyenye usajili wa kudumu, tukagundua kuwa wanachukua sera zetu na kuzibadili kidogo tu kuzifanya kuwa zao. “Si jambo baya kuiga kitu kizuri kutoka CCM, lakini ni kwa nini wananchi wachague kitu fotokopi wakati orijino kipo?” alihoji Rais Kikwete. Alisema wakati CCM ilipoingia madarakani ilitoa ahadi ya kutetea na kulinda Muungano, kuboresha ulinzi na usalama wa nchi, kuimarisha utawala bora ili kuhakikisha sheria na haki za binadamu vinafuatwa. “Kuboresha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, kuimarisha mihimili ya Dola ya Bunge, Mahakama na Utawala, kulinda uhuru wa kuabudu na wa vyombo vya habari, ahadi ambazo alisema zimetekelezwa kwa mafanikio makubwa. Kuhusu amani na utulivu, mgombea huyo alisema Watanzania wameendelea kuwa wamoja bila kubaguana kwa misingi ya dini, ukabila wala rangi na kwamba juhudi za kuwatenganisha zimegonga mwamba na kamwe hazitafanikiwa chini ya utawala wa CCM. “Uhalifu na ujambazi vimepungua sana, wakati tulipoingia madarakani, wimbi la ujambazi lilikuwa kubwa, lakini kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Polisi, ujambazi umepungua ingawa yapo matukio machache ya hapa na pale yanayojitokeza ambayo hata hivyo tunakabiliana nayo.” Alisema mapato ya Serikali yameimarika kutoka Sh bilioni 117.5 kwa mwezi mwaka 2005 hadi Sh bilioni 390 kwa mwezi hivi sasa, hatua ambayo alisema imepunguza utegemezi kutoka asilimia 42 hadi asilimia 28 na pesa hizo kwa kiasi kikubwa zinawafikia walengwa. Kuhusu rushwa, alisema Serikali ya CCM katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, imekuwa na dhamira ya dhati ya kukabiliana na vitendo vya rushwa kwa kuiongeza meno zaidi-Sheria ya Kupambana na Rushwa na kutungwa kwa Sheria ya Gharama za Uchaguzi na kuiboresha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). “Watu wote ni mashahidi namna watu tena wengine mashuhuri walivyofikishwa mahakamani, kutokana na kuhusishwa na rushwa. Tufanye nini zaidi ya hapa?” alihoji Kikwete. Rais Kikwete alisema pia Serikali ya CCM imeboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kupandisha mishahara ya watumishi. Alisema Serikali ilikuwa katika mgogoro na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) kutokana na kutaka malipo ya juu ya mishahara ingawa suala hilo limepatiwa ufumbuzi. “Kuhusu hili la mishahara si kama tunapuuza, tulichokubaliana nao ni kwamba tutalipa kwa kiwango tunachoweza na tusichoweza hatutalipa. Tumejitahidi pia kuboresha huduma nyingine muhimu kama maji, elimu, miundombinu, kilimo na afya. Tunaomba Watanzania watupigie kura katika uchaguzi mkuu ujao,” alimaliza Rais Kikwete. Awali kabla ya Rais Kikwete kuhutubia Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba alimkabidhi Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na kitabu cha Mwelekeo wa Sera za CCM ambavyo baadaye Rais Karume alimkabidhi mgombea, Rais Kikwete. Rais Karume, Makamba na mgombea mwenza wa urais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, walihutubia hadhira hiyo na kuwataka wananchi kuendelea kuichagua CCM. Wana-CCM walianza kuwasili katika viwanja vya Jangwani mapema asubuhi na hadi saa tano viwanja hivyo vilikuwa vimefurika umati mkubwa wa watu. Wana CCM waliitafsiri hali hiyo kuwa ni ishara na nyota njema kwao kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu mwaka huu. Kabla ya viongozi kuanza kutoa hotuba, bendi na vikundi mbalimbali vya burudani karibu vyote maarufu vilitoa burudani katika hadhara hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment