KAULI YA CCM KUHUSU KUANZISHWA KWA
CHAMA KIPYA CHA UPINZANI – CCJ
CHAMA KIPYA CHA UPINZANI – CCJ
Hivi karibuni vyombo vya habari vimekuwa vinaandika sana habari za kuanzishwa kwa Chamakipya cha upinzani kiitwacho Chama cha Jamii (CCJ). Habari kuhusu ujio wa chama hiki zimekuwa zinapambwa na vibwagizo vingi kwamba kimenzishwa na vigogo wa CCM kwa lengo la kukisambaratisha Chama cha Mapinduzi. Baadhi ya vyombo vya habari na hasa makala katika magazeti yamekuwa yanatabiri na kutarajia kumeguka kwa CCM kutokana na kuanzishwa kwa CCJ.
Chama cha Mapinduzi kinapenda kuwaarifu WanaCCM na Watanzania kwa jumla kwamba.
Kwanza, Chama cha Mapinduzi ndicho kiliruhusu uanzishwe mfumo wa vyama vingi 1992; hii ilikuwa baada ya Watanzania 80% kutoa maoni kwamba mfumo wa chama kimoja (yaani CCM) uendelee, na 20% walitaka uanzishwe mfumo wa vyama vingi. CCM ilikuwa na sababu nzuri ya kuwasikiliza waliowengi (80%), yaani wengi wape!
Lakini kwa kutumia busara kubwa CCM ilitoa fursa ya Watanzania 20% waanzishe vyama vyao vya upinzani na wamekuwa wanavianzisha, hadi sasa vipo 17. Hivyo kuanzishwa kwa chama kipya cha upinzani cha 18 si jambo la ajabu; lakini magazeti yanalikuza mno jambo hili kwa lengo la kuuza magazeti yao na pia kuwatisha Watanzania na hasa WanaCCM kwamba CCM inameguka. Hila hizi ovu hazitofanikiwa!
Pili, Chama hicho kinachoandikwa sana magazetini ndio kwanza kimeomba usajili. Hakijasajiliwa; na inawezekana kisipate usajili kabisa. Kwa mujibu wa sheria chama kinachoomba usajili, kwanza hupata usajili wa muda, na kisha huchukua miezi sita kupata usajili wa kudumu iwapo kitatimiza masharti na vigezo vya usajili wa kudumu. CCJ hawajapata hata usajili wa muda! Kwa kuwa mchakato wa uteuzi wa wagombea utaanza mara tu Bunge litakapovunjwa mwezi Julai, hao vigogo wa CCM watakao hama na kujiunga na CCJ wataomba uteuzi kupitia CCJ wakati gani? Hivyo taarifa kwamba kuna vigogo wengi wa CCM watagombea kupitia CCJ ni uvumi usio na mantiki yoyote. Hakuna kiongozi makini wa CCM atagombea Ubunge au Urais kupitia Chama kisicho na usajili; ni sawa na kuingia katika boti iliyotoboka na kutaka kusafiri nayo baharini!
Tatu, Hata kama ikitokea miujiza CCJ ikapata usajili wa kudumu kabla ya miezi sita na kuingia katika uchaguzi, na hata ikitokea baadhi ya viongozi wa CCM wakaamua kuhama CCM na kugombea kupitia CCJ, halitakuwa tukio la kwanza, wala sio jambo la ajabu. Tukio kama hilo limetokea mara nyingi. Wapo viongozi wengi wa vyama vya upinzani ambao walikuwa viongozi wakubwa CCM; waliamua kuhama, lakini CCM iliendelea kuwepo na iliendelea kuwa imara. Utabiri kwamba baadhi ya vigogo wa CCM wakihamia CCJ utakuwa ndio mwisho wa CCM, unapingwa na historia. Ukweli ni kwamba viongozi waliohama CCM na kwenda upinzani hawakupata mafanikio yoyote huko walikokwenda, wakati CCM waliodhani ingetetereka inaendelea kuwa imara, haijameguka wala kutetereka. Vivyo hivyo ikitokea baadhi ya viongozi wa CCM wakihama na kwenda CCJ au chama chochote cha upinzani, ukweli wa historia utabaki pale pale kwamba CCM itabaki imara, haitameguka wala kusambaratika; bali wao watakuwa wamejimaliza kisiasa. Ni muhimu Watanzania waelewe kwamba umaarufu wa viongozi wa CCM unatokana na umaarufu wa CCM, kiongozi anayeondoka CCM umaarufu wake huporomoka. Huu ndio ukweli wa kihistoria.
Nne, CCM inapenda kusisitiza kwamba wale wote wanaosubiri CCM imeguke wanapoteza muda wao. CCM ina historia ndefu na iliyotukuka, ina mtandao mpana sana, pia inajeshi kubwa la wanachama milioni nne na nusu. Sera za CCM za kupigania haki za wanyonge kuhusu elimu, afya, maji, uwezeshaji wananchi kiuchumi; ujenzi wa barabara za Vijijini na barabara kuu, n.k, zinawavutia watu wengi. Na jambo la muhimu ni kwamba zinatekelezwa vizuri pamoja na maneno ya ghiriba yanayoandikwa katika vyombo vya habari kwamba eti Rais Kikwete na CCM hawajafanya lolote! Hii ni ghiriba ambayo nayo haitafanikiwa. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita ambapo CCM ilipata ushindi wa 91% ni majibu tosha kwa wale wote wenye ndoto mbaya dhidi ya CCM. Matokeo haya ni salamu na ujumbe mzito kwamba wananchi Mijini na Vijijini wanaridhika na Sera za CCM na utekelezaji ilani ya CCM chini ya jemedari Rais Kikwete. Na ni hao hao wananchi watakaopiga kura katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu, na hapana shaka matokeo yatakuwa hayo hayo kwa CCM kuibuka na ushindi mkubwa. Katika mazingira haya ya Chama cha Mapinduzi kukubalika na kuheshimiwa na Watanzania, suala la kumeguka au kusambaratika ni ndoto ya mchana!
Tano, kwa kifupi CCM inapenda kuwatahadharisha WanaCCM kwamba wasitishike na ripoti za magazeti yanayokipamba chama ambacho hakina usajili, chama ambacho hakitashiriki katika Uchaguzi Mkuu ujao, wala hakuna kigogo hata mmoja wa CCM ambaye hadi sasa aliyejitambulisha kuwa ni mwanachama wa chama hicho. Kelele ni kubwa za kukipamba chama hiki (CCJ) kuliko hali halisi. Vitisho kwamba CCM itameguka ni vingi lakini ni uzushi mtupu. Hizi ni njama na ghiliba; hivyo WanaCCM na wananchi kwa jumla zipuuzeni. CCM ndiyo iliyoanzisha mfumo wa vyama vingi 1992 na hivi sasa vipo 17, haitishiki na hakijapata kutishika na mfumo wa vyama vingi; iweje hicho cha 18 ndicho kiinyime usingizi CCM! Tunatoa wito kwa WanaCCM kwamba tuendelee kujenga chama chetu, tuendelee kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa bidii. Chama cha CCJ ni chui wa karatasi, kisiwahangaishe, ni njama za kutufanya tuchelewe kutekeleza agenda muhimu za chama chetu na tubaki tunafuatilia chama ambacho bado hakina usajili na wala hakitashiriki katika uchaguzi. Tusiingie katika mtego huu uliowekwa na watu wasiokitakia mema chama chetu.
Mwisho kabisa tunapenda kuwahakikishia watanzania kwamba CCM hakikuogopa kuruhusu mfumo wa vyamba vingi, CCM ndiye mwasisi na mkunga wa mfumo wa vyama vingi, hivyo uanzishwaji wa chama chochote cha upinzani haliwezi kuwa tishio kwa CCM. Aidha kwa viongozi wa CCM kuhamia vyama vya upinzani sio jambo jipya na halijaathiri umaarufu na uimara wa CCM. Na mara nyingi viongozi wa CCM wanaohamia upinzani wamekuwa wanarejea CCM baada ya kugundua kwamba kwenye vyama vya upinzani hakuna lolote la maana, na CCM tumekuwa tunawapokea na tutaendelea kuwapokea bila ya kinyongo. Kwa jumla tunawaomba WanaCCM wasitishwe na ghiriba za magazeti kwani chama chetu bado ni imara na tumaini na nguzo ya Watanzania katika kudumisha umoja na amani ya nchi yetu.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na
CAPT JOHN Z. CHILIGATI (MB)
KATIBU WA NEC: ITIKADI NA UENEZI
CAPT JOHN Z. CHILIGATI (MB)
KATIBU WA NEC: ITIKADI NA UENEZI
No comments:
Post a Comment