Kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika Dar es Salaam tarehe 20/1/2011 chini ya Uenyekiti wa CCM Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, ilijadili kwa makini suala la mahitaji ya Katiba mpya na imetoa kauli ifuatayo
Kamati Kuu ina mpongeza Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano Dr. Jakaya M. Kikwete kwa kuzingatia ukweli kwamba Katiba iliyopo imefanya kazi vizuri kwa miaka 50, na hivyo kuelekeza kwamba ni kipindi kizuri cha kuitazama upya ili hatimaye ipatikane Katiba itakayotupeleka miaka 50 mingine ijayo.
Aidha, Kamati Kuu ina muunga mkono Mhe. Rais kwa hatua anayotarajia kuichukua ya kuunda Tume ya Kikatiba itakayokusanya maoni ya wananchi kuhusu masuala ya Katiba (Constitutional Review Commission). Kamati Kuu imesisitiza kwamba Tume hiyo ya Katiba iwe na mchanganyiko wa wananchi wa aina mbalimbali kama: wasomi, wakulima, wafanyakazi, Wafanyabiashara, Madhehebu ya dini, Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), pia makundi maalum kama vijana, wanawake, watu wenye ulemavu n.k. Aidha wakati ukifika wa Tume kuanza kazi itafaa ipewe muda wa kutosha ili ikusanye maoni mengi iwezekanavyo kutoka kwa wananchi wengi iwezekanavyo.
Kamati Kuu ilisisitiza mambo mengine yafuyatayo:-
· Kwamba elimu kwa umma kuhusu Katiba ya sasa itolewe ya kutosha ili kuwawezesha wananchi waelewe na ndipo watoe maoni wakiwa na uelewa kuhusu yaliyomo katika Katiba ya sasa.
· Kwamba Serikali itazame uwezekano wa kulishirikisha Bunge ili litunge sheria itakayoongoza utendaji kazi wa Tume ya Katiba, pamoja na kuelekeza Hadidu za Rejea za kazi ya Tume hiyo.
· Zoezi la kutoa elimu kwa umma kuhusu Katiba, na lile la Tume kukusanya maoni ya wananchi yapewe muda wa kutosha ili wananchi wengi iwezekanavyo watoe maoni yao kuhusu mambo gani yawemo katika Katiba ijayo.
· Kwamba mjadala kuhusu mambo gani mapya yaingie katika Katiba ijayo, na mambo gani yaliyomo katika Katiba ya sasa yaondolewe na yepi yabaki, sharti ufanywe kwa makini sana, bila jazba na bila ya vitisho wala mashinikizo kutoka kwa mtu yeyote au kikundi cho chote.
Kwa kifupi Kamati Kuu inawataka wananchi wajiandae kushiriki kwa ukamilifu katika mchakato wa mjadala kuhusu Katiba. Hii ni haki yao ya msingi. Jambo la kuzingatia ni kwamba mjadala huu uendeshwe katika hali ya amani na utulivu kama ilivyo jadi ya nchi yetu.
Imetolewa na:-
Capt. (Mst) John Z. Chiligati (Mb.),
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
ITIKADI NA UENEZI
No comments:
Post a Comment