Thursday, October 22, 2009

Makala: Siasa za Ushindani na Mustakabali wa Taifa

Na Mhe. Pius Msekwa,

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara)

Malengo na Changamoto za siasa za Ushindani.
1. Malengo

1.1 Baada ya mchakato mrefu wa maandalizi yake, hatimaye tarehe 1 Julai, 1992, Tanzania ilirejea katika mfumo wa siasa za ushindani baina ya vyama mbalimbali vya siasa.

Hatua ya kwanza ya mchakato huo ilichukuliwa mwezi Februari 1991, ambapo Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi, katika mkutano wake wa Februari, 1991, “baada ya kutafakari kwa makini suala la mageuzi yaliyokuwa yanatokea katika Afrika na duniani kote kwa jumla, iliamua uanzishwe mjadala wa kitaifa juu ya suala la ama kuendelea na mfumo wa chama kimoja cha siasa, au kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini Tanzania”.

Katika kutekeleza uamuzi huo, mnamo mwezi Machi, 1991, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitangaza kuundwa kwa Tume ya kuratibu mjadala wa kitaifa juu ya hoja hiyo (Tume ya Nyalali); na baada ya hapo kuishauri serikali kama ambavyo Tume hiyo itaona kuwa inafaa.

Tarehe 11 Desemba mwaka huo huo, Tume hiyo iliwasilisha kwa Rais taarifa yake ya awali, ikipendekeza mabadiliko yafanyike ya kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa. Tarehe 16 Januari, 1992, Tume iliwasilisha kwa Rais taarifa yake ya mwisho yenye mapendekezo kamili kuhusu hadidu zote za rejea ambazo Tume hiyo ilikuwa imepewa.

Rais naye aliwasilisha mapendekezo hayo ya Tume kwenye vikao husika vya Chama Cha Mapinduzi. Hatimaye Mkutano Mkuu maalum wa Chama Cha Mapinduzi uliofanyika mjini Dar es Salaam tarehe 18 hadi 19 Februari, 1992, ulipitisha azimio la kukubali kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

1.2 Changamoto kubwa wakati huo ilikuwa ni suala la ufinyu wa demokrasia. ‘Mageuzi’ ambayo Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM “iliyatafakari kwa makini” katika mkutano wake wa Februari 1991, yalikuwa ni mageuzi ya kutoka mfumo wa chama kimoja cha siasa, ambao ulikuwa umetawala katika nchi nyingi za Afrika na Ulaya ya Mashariki wakati huo, na kuingia katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa. Mageuzi hayo katika nchi za Afrika yalichochewa na wimbi kubwa la mageuzi ya kisasa lililozikumba nchi za Ulaya Mashariki katika kipindi hicho, ambazo zilikuwa chini ya mfumo wa chama kimoja cha kikomunisti, ambayo yalifikia kilele chake mwaka 1989.

Lakini pamoja na kuchochewa hivyo na mageuzi yaliyotokea katika nchi za Ulaya Mashariki, zilikuwapo vile vile sababu nyingine za ndani ya nchi hizi, ambazo pia zilichangia kuibuka kwa madai ya kutaka kufanyika kwa mageuzi ya mfumo wa kisiasa.

Kwa upande wa Tanzania, sababu hizo ni pamoja na matatizo makubwa ya kiuchumi, ambayo watu wengi walihisi kuwa yalisababishwa na ukiritimba wa mfumo uliokuwapo wa chama kimoja cha siasa na sera zake za ukiritimba katika uchumi.

2. Changamoto
Changamoto za woga wa kuingia katika siasa za ushindani:
Changamoto kubwa iliyojitokeza katika mjadala wa mabadiliko hayo, ilikuwa ni hofu, au woga, kuhusu mabadiliko yenyewe. Katika taarifa yake kwa Rais, Tume ya Nyalali ilieleza kwamba “wengi waliopendelea kuendelea na mfumo wa sasa wa chama kimoja, walikuwa na woga wa kuchagua kitu wasichokijua” (fear of the unknown). Tume hiyo ilihisi kwamba hiyo ndiyo sababu kubwa iliyosababisha asilimia themanini (80%) ya wananchi wote waliohojiwa na Tume hiyo wachague kuendelea na mfumo wa chama kimoja cha siasa. Lakini kwa busara zake, bado Tume hiyo ikapendekeza kwamba yafanyike mabadiliko ya mfumo huo. Na Chama cha Mapinduzi, kwa busara zake, kikakubali pendekezo hilo.

Hata hivyo, woga huo haukuwa kwa wananchi peke yao, kwani hata baadhi ya Hadidu za Rejea zenyewe zilionyesha dalili za wasiwasi, endapo Tume itapendekeza yafanyike mabadiliko ya mfumo wa siasa. Kwa mfano, Tume ilielekezwa:

(i) “Kutoa ushauri na mapendekezo juu ya haja, hekima, na matokeo ya kuendelea na chama kimoja cha siasa, au kubadili mfumo huo kwa kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa bila kuathiri malengo muhimu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za serikali, pamoja na haki na wajibu muhimu katika jamii”.

(ii) Kuzingatia, kuchambua, na kufafanua athari au manufaa ya mabadiliko yoyote yale katika mfumo uliopo, hasa kuhusu Muungano wetu, umoja wa Watanzania, amani ya nchi na maelewano yaliyopo miongoni mwa Watanzania wote bila kujali kabila, dini, rangi au jinsia yao.

(iii) “Kupendekeza njia za Kikatiba, kisheria na kisiasa za kujikinga na athari zozote za kisiasa au za kiusalama za kubadili au kutobadili mfumo wetu wa siasa, kwa shabaha ya kulinda umoja wa Taifa letu, Muungano wa nchi yetu na maelewano ya Watanzania wote bila kujali kabila, dini rangi au jinsia yao”.

(iv) “Kuzingatia na kufafanua athari za mabadiliko yoyote, endapo yatapendekezwa na Tume, katika suala zima la nafasi ya Zanzibar katika Muungano; na pia kuangalia kwa undani kama itakuwa ni kwa faida (salama) ya Zanzibar kutekeleza mabadiliko ya mfumo uliopo wa kisiasa, kwa kuzingatia historia ya kisiasa ya Zanzibar pamoja na tabia ya watu wa Zanzibar”.

Ukiyaangalia kwa undani zaidi, maelekezo hayo yanaashiria kuwapo kwa wasiwasi juu ya kubadilisha mfumo uliokuwapo, kwani yanasisitiza “kuchambua na kufafanua athari za mabadiliko hayo” na “kupendekeza njia za kikatiba. Kisheria na kisiasa, za kujikinga na athari za kisiasa au kiusalama za kubadili mfumo wetu”.

Lakini hofu kubwa zaidi ilikuwa ni kwa upande wa Zanzibar. Ndiyo sababu Tume ilielekezwa “kuangalia kwa undani kama itakuwa ni kwa faida (salama) ya Zanzibar kutekeleza mabadiliko ya mfumo uliopo, kwa kuzingatia historia ya kisiasa ya Zanzibar na tabia ya watu wa Zanzibar”. Maelekezo hayo yanaashiria kushinikiza kwamba Zanzibar isihusishwe katika mabadiliko ya mfumo wa kisiasa, kutokana na hofu hizo zilizotajwa.

Tume ya Nyalali inastahili kupongezwa kwa kazi yake nzuri iliyowezesha mabadiliko ya mfumo kufanyika kiulaini, kutokana na mapendekezo yake mazuri ya hatua za kuchukuliwa ili kujikinga na athari zile zilizokuwa zimehofiwa kuwa zingetokea. Tume ya Nyalali ilipendekeza kama ifuatavyo:

(1) Ili kulinda na kuhifadhi demokrasia, umoja, hali ya amani, utulivu wa kisiasa na mshikamano wa Taifa letu zitungwe sheria zitakazohakikisha kwamba:-

(a) Uandikishwaji wa vyama vya siasa nchini uwe ni jambo la Muungano.

(b) Vyama vya siasa viwekewe masharti maalum ambayo yatazingatia maslahi ya Taifa, hususan:

· Viwe ni vyama vya kitaifa (kwa maana ya pande zote mbili za Muungano); na visiwe vyama vyenye mwelekeo wa kugawa nchi au wananchi kwa msingi wa ukabila, dini, kanda, jinsia, rangi, au upande mmoja wa Muungano.

· Viwe ni vyama vinavyoanzishwa na wananchi wenyewe wenye nia ya kushirikiana katika kulinda matunda ya uhuru, na kuleta maendeleo zaidi ya nchi yetu.

· Viwe ni vyama vyenye lengo la kuendeleza na kuimarisha Muungano wetu. Visiwe vyama vyenye nia ya kuvuruga au kuvunja Muungano huu.

· Viwe ni vyama vinavyokubali misingi ya usawa wa haki na heshima kwa raia wote wa Tanzania.

· Viwe ni vyama vinavyokubali kueneza siasa na sera zake kwa misingi ya hoja. Yaani visiwe vyama vinavyotumia uchochezi, fujo, au mabavu katika kufikia malengo yake.

Mapendekezo hayo yote yalikubaliwa na kuingizwa katika Katiba ya nchi, na vile vile katika Sheria ya Vyama vya Siasa, na. 5 ya 1992. Sheria hiyo pia ilitoa tafsiri sahihi ya chama cha siasa, kwamba;

“Political Party” means any organized group formed for the purpose of forming a government or a Local Government Authority within the United Republic through elections; and for putting up or supporting candidates for such elections”.

3. Changamoto baada ya kuingia katika siasa za ushindani:

Changamoto nyingine zaidi zimejitokeza katika uendeshaji wa mfumo huu wa siasa za ushindani. Miongoni mwake ni hizi zifuatazo:-

(1) Hali ya kuwa na ‘vyama vingi lakini sera moja’. Hii imekuwa ni changamoto kwa sababu nadharia ya ubora wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa inaeleza kwamba inawapatia wananchi ambao ni wapiga kura, fursa ya kuchagua chama chenye sera ambazo zinawavutia zaidi, na wangependa kukiweka chama chenye sera hizo madarakani ili kiweze kuzitekeleza. Lakini katika nchi maskini kama Tanzania, sera pekee itakayowanufaisha wananchi wote, ni sera ya kuwaondoa katika dimbwi hilo la umaskini kwa kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Hakuna chama kinachoweza kuwa na sera ambayo ni tofauti na hiyo.

Matokeo yake ndiyo hayo ya ‘vyama vingi, sera moja’. Kwa hiyo wananchi wanakosa fursa ya kuchagua sera iliyo bora zaidi miongoni mwa sera za vyama mbalimbali vilivyopo. Kutokana na hali hiyo, uchaguzi unakuwa ni zoezi tofauti na lile linaloelezwa katika nadharia ya demokrasia ya vyama vingi.

(2) Hali ya kutokuwa na chama ambacho kinaweza wakati wowote kuunda ‘serikali mbadala’, kutokana na nguvu yake ilivyo ndani ya Bunge, kwa maana ya wingi wa Wabunge wake.

Nadharia nyingine ya ubora wa demokrasia ya vyama vingi inasema kwamba wakati wote unakuwapo uwezekano wa kuunda serikali mbadala, endapo serikali iliyopo madarakani itakuwa imeondolewa madarakani kwa kura za Wabunge walio wengi. (vote of no confidence).

Tukio la aina hiyo liliwahi kutokea Uingereza mwaka 1979, wakati serikali iliyokuwa imeundwa na chama cha Labour Party ilipoondolewa kwa kura za Wabunge 311 waliosema ‘ndiyo’ kwa hoja ya kuiondoa serikali hiyo madarakani; dhidi ya kura 310 za Wabunge waliosema ‘hapana’. Hivi karibuni, Serikali ya India pia ilipata mtihani kama huo, lakini iliweza kupata kura za ushindi na kubaki madarakani.

Hapa kwetu, matokeo ya kura katika awamu tatu za uchaguzi mkuu tangu tulipoingia katika mfumo wa siasa za ushindani, yanaonyesha kwamba nguvu ya upinzani Bungeni imekuwa ikizidi kupungua katika kila uchaguzi mkuu. Nguvu ya vyama vya upinzani vyote kwa pamoja ndani ya Bunge baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995, ilikuwa ni chini kidogo ya 20% ya viti vyote vya majimbo Bungeni, kwani CCM ilipata 80.17% ya viti hivyo.

Katika uchaguzi mkuu uliofuatia wa mwaka 2000, CCM ilipata 87.5% ya viti vyote vya majimbo Bungeni; na katika uchaguzi mkuu wa tatu wa mwaka 2005, CCM ilipata 88.8% ya viti vyote vya majimbo Bungeni.

Hali hiyo inaashiria mambo mawili, kwamba:-

(a) Serikali ya CCM haiwezi kuondolewa madarakani kwa kura za Wabunge walio wengi (majority) wanaotaka kuiondoa madarakani, kwa sababu hawapo; na

(b) Hata kama vikiamua kushirikiana, vyama vya upinzani bado havina idadi ya Wabunge wa kutosha kuviwezesha kuunda serikali mbadala.

Hata hivyo, suala la ushirika siyo rahisi katika jambo hili. Wakati fulani baadhi ya vyama vya siasa vya India vilijaribu kuungana ili kuunda serikali, baada ya kukosekana chama chochote ambacho kilipata idadi ya kutosha ya wabunge kukiwezesha kuunda serikali peke yake. Vyama vilivyokubaliana kuungana bado havikuwa na idadi ya kutosha ya Wabunge, kwa hiyo wakajaribu kuunda ‘serikali ya wachache’ (minority government). Serikali hiyo ilikaa madarakani kwa muda wa siku 13 tu kabla Bunge jipya halijakutana. Katika muda huo, walijaribu kupata washirika wengine, lakini wakashindwa. Mwandishi mmoja wa mambo ya kisiasa huko India aliukejeli muungano wao huo kwa kusema:

“It was like a cemetery. Those who were inside could not come out, and those who were outside had no wish to go in”.

4. Changamoto ya mfumo wa uchaguzi:

Kwa upande wa uchaguzi, Tanzania inaendelea kutumia mfumo wa uchaguzi tuliorithishwa na Waingereza, ambapo kila chama cha siasa kinasimamisha wagombea wake katika kila jimbo la uchaguzi, endapo kina uwezo wa kufanya hivyo.

Mfumo huo una matatizo mawili. Kwanza, ni kwamba katika macho ya wapiga kura wengi, mfumo huo haushindanishi vyama vya siasa, bali unashindanisha watu wanaogombea uchaguzi huo. Ndiyo sababu katika baadhi ya majimbo, imewahi kutokea kwamba mgombea aliyejaribu kusimama kwa tiketi ya CCM lakini akokosa uteuzi wa chama hicho, anashauriwa na wapiga kura ahamie chama kingine chochote ili waweze kumchagua. Na kweli anachaguliwa kwa tiketi ya chama hicho alichohamia. Hii inamaanisha kwamba wapiga kura hao wanamtaka huyo mtu, na siyo chama chake! Ndiyo sababu wanamshauri ahamie chama kingine chochote, bila kujali ni chama gani.

Pili, ni kwamba kwa sababu hiyo ya kushindanisha watu badala ya kushindanisha vyama, mfumo huo unatoa mwanya kwa wenye uwezo mkubwa wa fedha, kutumia fedha zao kujinunulia ushindi. Kwa maneno mengine, mfumo huo unatoa mwanya kwa rushwa kutumika katika uchaguzi.

Tatu, uzoefu wa awamu tatu za uchaguzi mkuu zilizopita, unaonyesha kwamba baadhi ya vyama vinashindwa kusimamisha wagombea katika majimbo yote 232 yaliyopo, zaidi kwa sababu ya gharama zake kuwa kubwa, miongoni mwa sababu nyingine.

Kwa ajili hiyo, tayari yapo mawazo miongoni mwa wananchi, kwamba pengine ingefaa tufikirie uwezekano wa kutumia mfumo wa uwakilishi Bungeni unaotokana na uwiano wa kura za kila chama cha siasa (proportional representation). Katika kanda ya SADC, mfumo huo ndio unaotumika Msumbiji, Afrika Kusini na Namibia, miongoni mwa nchi nyingi nyingine, hasa za Ulaya. Ni mawazo ambayo yanastahili kufanyiwa kazi kwa kupima na kulinganisha uzuri na ubaya wake, ili ukionekana kuwa unafaa, uweze kutumika pia katika nchi yetu.

5. Changamoto ya siasa za ushindani Zanzibar:

Tumekwisha kutaja mapema katika makala haya, ile hofu iliyoelezwa katika hadidu za rejea za Tume ya Nyalali, kwa kuitaka Tume hiyo “kuzingatia kwa undani kama itakuwa ni kwa faida (salama) ya Zanzibar kutekeleza mabadiliko ya mfumo wa kisiasa uliopo, kwa kuzingatia historia ya kisiasa ya Zanzibar, na tabia za watu wa Zanzibar”.

Ni kweli kwamba utekelezaji wa siasa za ushindani baina ya vyama vya siasa umeleta mgogoro katika utawala wa Zanzibar, ambapo kila uchaguzi mkuu umefuatiwa na vitendo vya ghasia kutokana na chama cha CUF kutokutambua matokeo ya uchaguzi huo. Mazungumzo ambayo yamekuwa yakifanyika baina ya vyama vya CCM na CUF yaliwezesha kupatikana kwa MUAFAKA I na II; lakini matatizo ya kisiasa bado yanaendelea. Kwa hiyo juhudi za kutafuta MUAFAKA III vile vile zinaendelea.

6. Mwisho

Katika kuhitimisha makala haya, ni vema kutambua na kupongeza kuwapo kwa chombo rasmi cha mazungumzo kinachowaweka pamoja Wakuu (Wenyeviti na Makatibu Wakuu) wa vyama vyote vyenye Wabunge. Chombo hicho kinaitwa Tanzania Center for Democracy (TCD), na kinashirikisha pia Wakuu wa vyama vingine vyenye usajili wa kudumu, ambavyo kwa wakati uliopo havina wabunge. Kuwapo kwa chombo hiki ni hatua muhimu sana ya kujenga maelewano na ushirikiano baina ya vyama baada ya kumalizika kwa uchaguzi.

Mantiki yake ni kwamba wakati wa uchaguzi ni wakati wa ushindani mkali, kwa kila chama kuwania kupata kura nyingi iwezekanavyo. Lakini baada ya uchaguzi mkuu kumalizika, ni jambo zuri sana kwamba tumeweza kuwa na chombo kama hicho cha ushirikiano baina ya vyama vya nje ya Bunge. Na kama ambavyo vyama vyenyewe vyenye Wabunge vinapata ruzuku kutoka serikalini, chombo hiki pia kinapata ruzuku kutoka serikalini kusaidia uendeshaji wa shughuli zake.


Mungu ibariki Tanzania

No comments: