Tuesday, 02 November 2010 02:23
Dk Shein akizungumza na wananchi wa Zanzibar mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya UraisFidelis ButaheCCM jana ilifanikiwa kunyakua tena kiti cha urais baada ya mgombea wake, Dk Ali Mohamed Shein kuibuka mshindi kwenye uchaguzi uliofanyika Jumapili akimshinda mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad.Dk Shein, ambaye anamalizia kipindi chake kama makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano, sasa anakuwa rais wa saba wa Zanzibar, ambayo inaundwa na visiwa vya Pemba na Unguja akimbadili Abeid Amani Karume pia wa CCM.Lakini Dk Shein atakuwa na changamoto kubwa ya kuwa kiongozi wa kwanza kuongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa na atashirikiana na Maalim Seif, ambaye kwa mujibu wa marekebisho ya katiba baada ya kufikiwa kwa maridhiano, anakuwa makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar.Akitangaza matokeo hayo, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Khatib Mwinyichande alisema Dk Shein alipata kura 179,809 ambazo ni sawa na asilimia 50.1.Kwa mujibu wa matokeo hayo, Maalim Seif, ambaye amegombea urais kwa mara ya nne, alipata kura 176,338 ambazo ni sawa na aslimia 49.1 ya kura zote 358,815.Alisema kuwa vyama vilivyosimamisha wagombea urais katika uchaguzi huo ni pamoja na AFP, CCM, CUF, Jahazi Asilia, NCCR-Mageuzi, NRA na Tadea."Matokeo yanaonyesha kuwa mgombea wa NRA amepata kura 480 sawa na asilimia 0.1, wa CCM kura 179,809 sawa na asilimia 50.1, wa CUF kura 176,338 sawa na asilimia 49.1, Jahazi Asilia kura 803 sawa na asilimia 0.2, NCCR kura 363 sawa na asilimia 0.1, NRA kura 525 sawa na asilimia 0.1 na Tadea kura 497 sawa na asilimia 0.1," alisema Mwinyichande.Tofauti na ilivyokuwa kwenye chaguzi zilizopita, jana hali ilikuwa shwari wakati mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) akitangaza matokeo ya urais. Shangwe zilizofuata baada ya Dk Shein kutangazwa kuwa mshindi, hazikunakshiwa kwa vijembe vya kuudhi wapinaani kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye chaguzi zilizopita.Hata Maalim Seif alikuwepo wakati wa hafla hiyo na akakubali kwenda mbele kutoa hotuba ya kukubali matokeo ambayo ilijaa hekima na busara ikieleza umuhimu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande hizo mbili kuu, huku ikitaharidha kuhusu vitendo vinavyoweza kuvuruga maridhiano hayo."Kwa mara ya kwanbza uchaguzi umefanyika kwa amani, bila ya vitisho. Kampeni ziliendeshwa kiungwana na kwa ustaarabu," alisema Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa waziri kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)."Nachukua nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa Dk Ali Mohamed Shein kwa kupata ridhaa ya Wazanzibari atuongoze kwa miaka mitano inayokuja."Dk Shein ana uwezo, uzoefu na mahaba kwa nchi yake. Tunatumaini ataongoza kwa busara na hekima kwa lengo la kuunganisha nchi yetu. Naamini kuwa Wazanzibari walifanya maamuzi sahihi Julai 31. Tarehe hiyo waliamua kuunda serikali shirikishi."
Dk Shein na Mr Seif wakipongezana mara baada ya tume ya uchaguzi kutoa matokeoSeif, ambaye alikuwa akizungumza kwa utulivu, alisema uamuzi huo umeweka enzi mpya ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kwamba Wazanzibari wamempa Dk Shein jukumu la kuongoza kwa mara ya kwanza serikali ya umoja.Lakini mkongwe huyo wa siasa visiwani Pemba na Unguja hakusita kutoa tahadhari kwa Dk Shein na CCM wakati akitaja mambo makuu matatu muhimu."Kwanza ni shukrani kwa Tume ya Uchaguzi kwa kuendesha uchaguzi ambao ulikuwa na afadhali kulinganisha na chaguzi nyingine," alisema."Lakini kuna dosari ambazo ni lazima zirekebishwe. Mwenye matatizo si wewe mkurugenzi... ni baadhi ya maofisa wako."Alieleza matatizo ambayo maofisa wa uchaguzi wamekuwa wakiyafanya akisema yanasababisha watu wasiwe na imani na tume."Jambo la pili ni kwamba Dk Shein ni rais mteule. Ametangazwa tu kuwa mshindi, lakini hakuna mshindi. Washindi ni Wazanzibari wote na Shein ni mteule tu."Dk Shein alionya katika suala lake la tatu kuwa baada ya matokeo hayo kusiweo na siasa za kubezana."Siasa za kubezana zitachafua hali ya hewa kabisa," alionya Maalim Seif akimtaka Dk Shein afikishe ujumbe huo kwa viongozi wenzake wa CCM na wanachama wao.Naye Dk Shein, ambaye huzungumza kwa utaratibu na mpangilio, alimshukuru Maalim Seif kwa hotuba yake, aliyoielezea kuwa ilijaa busara na hekima na kuahidi kutekeleza yote ambayo kiongozi huyo wa CUF aliyazungumzia."Nafahamu fika kuwa kazi hii ni nzito... Mungu anisaidie, anipe hekima na busara ili niifanye kwa uadilifu," alisema Dk Shein.Shein sasa atakuwa na changamoto jipya la kuwa rais wa kwanza kuongoza Zanzibar akishirikiana na chama kikuu cha upinzani, CUF baada ya pande hizo mbili kufikia maridhiano ambayo yalilifanya Baraza la Wawakilishi kuridhia kupitisha sheria inayoruhusu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.Kwa mujibu wa muundo mpya wa Serikali ya Zanzibar, mshindi wa uchaguzi mkuu ndiye ataingia Ikulu akiwa rais na mgombea aliyeshindwa atakabidhiwa nafasi ya makamu wa kwanza wa rais.Muafaka huo ulifikiwa baada ya viongozi wakuu wa vyama hivyo viwili, Rais Amani Abeid Karume kukutana kwa faragha Ikulu na katibu mkuu wa CUF, Seif Sharrif Hamad Novemba 4, 2009.
Taarifa iliyotolewa baada ya faragha hiyo ilieleza kuwa wawili hao walizungumzia haja ya kudumisha amani na utulivu pamoja na kuwa na maelewano na ushirikiano baina ya wananchi wote wa Zanzibar.
Source: Mwananchi