MAAMUZI YA KIKAO CHA HALMASHAURI KUU YA TAIFA (NEC)
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM katika kikao chake cha leo (7/3/2009) kilichofanyika chini ya Uenyekiti wake Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete imefanya maamuzi yafuatayo:-
Kuhusu Kura za Maoni Kuwapata Wagombea Nafasi katika Vyombo vya Dola (Ubunge/Uwakilishi/Udiwani)
Kwa kutimiza azma ya kupanua demokrasia ndani ya Chama, na pia kwa lengo la kumshirikisha kikamilifu kila mwana CCM katika kupiga kura za maoni za kuwapata wagombea viti vya Ubunge, Baraza la Wawakilishi na Udiwani, Halmashauri Kuu ya Taifa imeamua kwamba kila mwana CCM atakuwa na haki ya kupiga kura za maoni kupitia Tawi lake.
Utaratibu huu utaanza kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani (2010) na unafuta utaratibu wa zamani ambapo kura za maoni zilikuwa zinapigwa na wajumbe wachache kupitia mikutano mikuu ya Majimbo.
Utaratibu wa kura za maoni utakuwa kama ifuatavyo:-
(a)Kabla ya kura za maoni, wagombea watapata fursa ya kutembelea matawi yote na kukutana na wana CCM kwa lengo la kujitambulisha na kuomba kura.
(b) Ziara hizi zitaandaliwa na CCM ngazi ya Wilaya na wagombea watasafiri kwa pamoja kwa usafiri ulioandaliwa na kugharamiwa na CCM. Hatua hii ina lengo la kutoa haki sawa kwa kila mgombea kutembelea matawi yote na kujitambulisha.
(c) Baada ya ziara ya kujitambulisha kukamilika itapangwa siku moja ambapo wanachama wote watapiga kura kwenye matawi yao. Upigaji kura utaanza saa 2 asubuhi hadi saa 8 mchana Kamati ya Siasa ya Tawi itaweka utaratibu wa kuhakiki zoezi hili. Kura zitahesabiwa katika kituo husika na matokeo kutangazwa siku hiyo hiyo. Nakala ya matokeo itabadikwa hadharani nje ya ofisi ya Tawi, au mahali ambapo kura zitapigiwa ili yawe wazi. Kila mgombea atakuwa na haki ya kuweka wakala wa kusimamia upigaji kura, na zoezi la kuhesabu kura. Wilaya itaweka wasimamizi wa uchaguzi katika kila Tawi.
(d) Baada ya kura kuhesabiwa katika kituo na matokeo kutangazwa, msimamizi wa kituo atatakiwa kupeleka matokeo hayo kwa Katibu wa CCM (W) kwa njia yo yote ya haraka kwa mfano simu, fax, pikipiki, n.k.
(e) Baada ya matokeo kutoka matawi yote kufika wilayani, Katibu wa CCM (W) akisimamiwa na Kamati ya Siasa ya Wilaya atajumlisha kura za kila mgombea. Wakati wa zoezi la kujumlisha kura, kila mgombea atakuwa na haki ya kuwepo mwenyewe au mwakilishi wake.
(f) Baada ya zoezi la kura za maoni kukamilika, vikao vya ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa vitakaa kuchambua kwa undani zaidi sifa za wagombea na kuzingatia kura za maoni walizopata, na hatimaye kuteua wagombea. Majina ya wagombea hatimaye yatawasilishwa kwenye Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi na ratiba ya Tume ya Uchaguzi.
Halmashauri Kuu ya Taifa inaamini kuwa utaratibu huu unatoa nafasi kwa kila mwana CCM kushirikishwa katika mchakato wa kuwapata wagombea na pia watashiriki kuwaunga mkono wagombea wa CCM ili wapate ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu. Vile vile utaratibu huu utaondoa tabia mbaya iliyojitokeza huko nyuma ya baadhi ya wagombea kutoa rushwa kwa wapiga kura ili kujipatia ushindi kwani kwa utaratibu huu haitakuwa rahisi kuwahonga wana CCM wa matawi yote Jimboni bila ya kubainika.
Aidha, Halmashauri Kuu imeagiza Kamati za Usalama na Maadili katika ngazi zote ziwe macho wakati wa kura za maoni ili kubaini vitendo vya rushwa. Mgombea ye yote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya kutoa rushwa au kukiuka kanuni za uchaguzi, ataenguliwa katika kugombea, na iwapo atajihusisha na rushwa atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Kuhusu Utaratibu wa Kuongeza Wabunge/Wawakilishi Wanawake Kufikia Lengo la Asilimia 50
Halmashauri Kuu ya Taifa baada ya kuchambua njia mbalimbali za namna bora ya kuwapata Wabunge/Wawakilishi Wanawake ili kufikia lengo la asilimia 50 lililowekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, imeamua kama ifuatavyo:-
(a) Halmashauri Kuu ya Taifa imependekeza kwa Serikali kuwa idadi ya Wabunge katika Bunge la Muungano iwe na ukomo wa viti 360. Hivyo fomula yo yote ya kuongeza idadi ya Wabunge Wanawake sharti izingatie ukomo huu.
(b) Kwamba tuendelee na utaratibu uliopo sasa wa kuwapata Wabunge/Wawakilishi wa Viti Maalum Wanawake. Isipokuwa kwamba idadi yao katika kila chombo ipatikane kutokana na asilimia 50 ya Wabunge/Wawakilishi wote wa majimbo yaliyopo (232).
(c) Kwa kuzingatia kwamba Bunge litakuwa na ukomo wa viti 360 na kwamba idadi ya majimbo ya uchaguzi yaliyopo sasa ni 232, idadi ya Wabunge Wanawake itakayopatikana ni 116 sawa na asilimia 50 ya Wabunge wote wa Majimbo. Hata hivyo kuna Wabunge Wanawake 7 watapatikana kwa mujibu wa Katiba ya nchi; hivyo kwa utaratibu huu, Wanawake 109 ndio watakaopatikana kupitia Viti Maalum.
(d) Kwa upande wa Zanzibar, inapendekezwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iweke ukomo wa idadi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi iwe wajumbe 86. Kwa kuwa hivi sasa Baraza lina viti 50 vinavyotokana na majimbo ya uchaguzi, idadi ya Wawakilishi Wanawake watakaopatikana kwa njia hii itakuwa 25, yaani asilimia 50 ya Wawakilishi wote wa kuchaguliwa katika majimbo yaliyopo kwa kuwa Wawakilishi Wanawake 5 watapatikana kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar; hivyo Wanawake 20 ndio watakaopatikana kutokana na Viti Maalum.
(e) Katika kuandaa orodha ya wagombea Wanawake kwa nafasi 109 za Bunge la Muungano, na nafasi 20 za Uwakilishi zitakazogombaniwa, watapigiwa kura na vikao vya UWT. Kwa hiyo wagombea Ubunge/Uwakilishi watapigiwa kura na Mkutano Mkuu wa UWT wa Mkoa. Vivyo hivyo wagombea Udiwani wa Viti Maalum Wanawake watapigiwa kura na Mkutano Mkuu wa UWT wa Wilaya.
(f) Halmashauri Kuu ya Taifa pia imezielekeza Serikali zote mbili zikuchukue hatua zifuatazo:-
(i)Serikali ya Muungano irekebishe Katiba ya nchi na sheria ya Uchaguzi ili kuweka ukomo wa idadi ya Wabunge katika Bunge la Muungano kuwa 360, na pia kuhalalisha kisheria utaratibu huu mpya wa kuwapata Wabunge Wanawake kupitia Viti Maalum.
(ii) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pia ibadilishe Katiba, na sheria ya Uchaguzi ili kuweka ukomo wa idadi ya Wawakilishi kuwa 86 na pia kuhalalisha kisheria utaratibu mpya wa kuwapata Wabunge Wanawake kuptia Viti Maalum.
(iii) Ili kuongeza idadi ya Wanawake katika Baraza la Wawakilishi, Katiba ya Zanzibar ifanyiwe marekebisho ili kumwezesha Rais wa Zanzibar ateue Wanawake wasiopungua watano (5) miongoni mwa nafasi kumi alizonazo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.
NEC inawahimiza na kuwahamasisha wanawake wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani kupitia Majimboni badala ya kutegemea viti maalum. Aidha, vyama vyote vya siasa vinahamasishwa na kuhimizwa viteue Wanawake wengi zaidi kugombea nafasi majimboni.Mwisho, Halmashauri Kuu ya Taifa imeipongeza Kamati Maalum iliyoongozwa na Dr. Bilal kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya katika kukusanya maoni haya ambayo yamekubaliwa rasmi na sasa yatawasilishwa Serikalini kwa utekelezaji.Kuhusu Uteuzi wa
Mwisho wa Majina ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya za UVCCM na UWT
Halmashauri Kuu ya Taifa imefanya uteuzi wa majina ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Vijana na Wanawake.
Waliofanyiwa uteuzi ni:-
1. Ndugu Martin Reuben Shigela - UVCCM
2. Ndugu Hasna Sudi Mwilima - UWT
Majina haya yatafikishwa katika Baraza Kuu la UVCCM na la UWT kwa ajili ya kupigiwa kura za uthibitisho.